Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao (katikati)
akimkabidhi jezi mmoja wa wawakilishi wa timu zinazoshiriki ligi daraja
la kwanza ya StarTimes (SFDL) wakati wa hafla ya kukabidhi jezi hizo
iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano. Kushoto akipiga makofi ni
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Malinzi.
(Picha na mpiga picha wetu).
Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao (Kushoto)
akimkabidhi jezi mmoja wa wawakilishi wa timu zinazoshiriki ligi daraja
la kwanza ya StarTimes (SFDL) wakati wa hafla ya kukabidhi jezi hizo
iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji
wa Bodi ya Ligi Kuu nchini, Bw. Boniface Wambura. (Picha na mpiga picha
wetu)
Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao (Kulia)
akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jezi kwa timu za Ligi Daraja la
Kwanza ya StarTimes (SFDL) iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano.
Katikati ni ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw.
Jamal Malinzi na wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Selestine
Mwesigwa.
Na Mwandishi Wetu.
KAMPUNI
ya Urushaji wa Matangazo Kidijitali ya StarTimes ya Tanzania imekabidhi
jezi kwa timu zinazocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Tanzania, ikiwa
ni moja kati ya udhamini wa ligi hiyo ijulikanayo kama Ligi Daraja la
Kwanza ya StarTimes (SFDL).
Akizungumza
na waandishi wakati wa kukabidhi jezi hizo jijini Dar es Salaam
Jumatano, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang
Liao alisema kuwa angependa kuona jezi hizo zinakuwa kama chachu ya
kufanya vizuri kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu.
“Kwanza
napenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ushirikiano huu
wanaouonyesha kwetu kama StarTimes, lakini leo hii tunatoa jezi kwa
timu za ligi hii ya daraja la kwanza ya StarTimes ikiwa ni sehemu ya
udhamini wetu mbali na udhamini wa fedha za uendeshaji.”
“Jezi
hizi sasa ni kama chachu ya timu zote za ligi daraja la kwanza kuongeza
bidii na kufanya vizuri katika ligi hii msimu huu ili kuvutia wadhamini
wengi zaidi. StarTimes kupitia udhamini huu tunaamini tumefungua njia
kwa wengine nao kujitokeza na pia kuinua ari ya timu hizi,” alisema Bw.
Liao.
Bw.
Liao alisema kuwa kutokana na jitihada hizo angependa kuona wachezaji
wanaocheza katika ligi hiyo wanacheza katika Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’
na timu nyingine kubwa kimataifa.
Kwa
upande wake mwakilishi wa Timu zinazoshiriki ligi hiyo, Bw Masao Bwire,
aliipongeza kampuni ya StarTimes kwa kujitokeza kuipiga jeki ligi hiyo
ambayo imekuwa ikiendeshwa bila udhamini wowote kwa kipindi kirefu.
Pamoja
na hayo pia alilipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa
jitihada zake za utafutaji wa wadhamini kwa lengo la kuinyanyua ligi
daraja la kwanza nchini ambayo imekuwa ikizalisha wachezaji wanaocheza
ligi kuu.
“Naipongeza
kampuni ya StarTimes kwa kujitokeza kudhamini ligi daraja la kwanza.
Hii ni hatua kubwa kwa ligi hii, kwa kuwa imekuwa ikienda bila udhamini
kwa muda mrefu. Kukosekana kwa udhamini kulikuwa kukisababisha timu
kutojiendesha vizuri hasa katika masuala ya vifaa, kulipa wachezaji na
viongozi posho, kusafiri mbali kwa ajili ya mechi na usajili.
Tunashukuru sana hayo sasa yatabakia historia na tunawaomba wadau
wengine wajitokeze kwani bado hitaji ni kubwa. Lakini pia naipongeza TFF
kwa jitihada zake kubwa za kutafuta wadhamini ili kusaidia maendeleo ya
ligi hii nchini,” alisema Bw. Bwire.
Naye
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Bw. Jamal Malinzi
aliishukuru kampuni ya StarTimes kwa ushirikiano inaoutoa ili
kuhakikisha ligi hiyo inasonga mbele na kuziasa timu zinazoshirki ligi
hiyo kuongeza jitihada na kufanya vizuri baada ya kupata msukumo huo
toka StarTimes.
“Napenda
kuishukuru kampuni ya StarTimes kwa ushirikiano inaotuonyesha ili
kuipeleka mbele ligi hii lakini pia naziasa timu zote zinazoshiriki ligi
hii ya StarTimes ya Daraja la Kwanza kuongeza jitihada na kufanya
vizuri katika msimu huu wa ligi. Pia ningependa kuwataka na nyinyi
mfanye juhudi kutafuta wadhamini wengine kwani mnaweza kufanya hivyo ili
kufanya ligi iwe na ushindani zaidi.” alihitimisha Bw. Malinzi.
No comments:
Post a Comment