Maboga yaliotengenezwa kwajili ya Maruhani
Na Swahilivilla blog. Washington D.C
Jana
ililkuwa ni "Siku ya Maruhani" nchini Marekani. Siku hii ijulikanayo
kama "Halloween" husherehekewa kila tarehe 31 Oktoba, na ina historia
ndefu.
Siku
ya Maruhani ilianzia huko barani Ulaya kiasi miaka 2,000 iliyopita
ikifungamana na imani za kishirikina. Wazung walipoyavamia mabara ya
Amerika walihamia pia na utamaduni mila, desturi, dini, na silka zao -
na sema upendavyo. Miongoni mwa hayo ilikuwa ndiyo hii siku ya Maruhani
ambayo jina lake la asili ni "Samhein".
Tuyaachie
ya historia kwa wanahistoria, lakini kwa ufupi hii iliaminika kuwa ni
siku ambayo pepo, majini, maruhani, mazimwi na mizimu au mizuka ya watu
waliokufa hurejea hapa duniani katika maeneo yao ya asili na
kujichanganya na watu waliohai.
Maudhui
kuu ya siku hii ni kutisha, kuadhibu na mauti, ingawaje katika enzi
zetu za leo imekuwa ni siku kuu ya watoto zaidi kuliko watu wazima.
Sherehe zake hufanyika kuanzia familia, mitaa, makazini na hadi kufikia
Ikulu yenyewe. Rejea kwenye toleo la jana la Swahilivilla uone Ikulu ya Marekani ilivyoadhimisha siku hii akiwepo rais Obama na familia yake.
Wana maruhani wakiwa katika kwaride. (Photo Jefferson Siegel/New York daily news)
Kama
ambavyo kila siku kuu au sherehe huwa zinaaambatana na ada maalum
ambazo zikikosekana basi siku hiyo huwa kana kwamba haijatimia, Siku ya
Maruhani nayo pia ina ada na desturi zake. Na kama zilivyo sherehe
nyingi hapa Marekani siku hii pia nayo imekuwa fursa ya wafanyabiashara
kujipatia rizki zao.
Mapambo:
Shamra shamra za Siku ya Maruhani huanza mapema, pengine tangu mwezi wa
Septemba kwa kuweka mapambo kwenye majumba, mabarabara na hata sehemu
za kazi na biashara.
Na
kama tulivyotangulia kusema, mapambo yote huwa yanalenga kwenye hali ya
kutisha, kuadhibu na mauti. Miongoni mwa mapambo hayo ni buibui na
nyumba zao, popo wakining'inia, mifupa na mabufuru ya vichwa vikiashiria
watu waliokufa, panga, paka weusi, masanamu ya mizuka au mazombi na
vimbwanga vyengine. Almradi kuonesha kuwa nyumba zimesibiwa na maruhani
(haunted house). Si hasha ukapita vichochoroni ukakutana na kitu
ukashtuka. Kwa ufupi ni kama vile tunavyoona kwenye picha za kutisha
(scary movies).
Maboga
nayo ni sehemu muhimu katika Siku ya Maruhani. Hukaushwa, kutobolewa
kwa mitindo maalum na kupakwa rangi na kuwa katika umbo la kutisha,
kisha kutiwa mshumaa ndani. Boga hili maarufu huitwa kandili ya Jack 'O
(jack-o’-lantern). Kiasili, mshumaa uliondani unaashiria roho iliyoko
kifungoni ikiadhibiwa.
Mavazi
(Costumes): Inaaminika kuwa Wazungu wa kale huko Ulaya, walikuwa
wakivaa mavazi ya kutisha katika siku hii ili kuwababaisha pepo, majini,
maruhani na mazimwi wanapokuja, wadhani kuwa ni wenzao na hivyo
kuwaacha na kutowadhuru. Kwa hivyo mpaka leo mavazi ya siku hii huwa ni
ya kutisha, na watu hutembea kama mizuka, mazimwi (mazombi) au mtu
aliyechagawa.
Makazini
watu huruhusiwa kuvaa mapambo maalum ya kutisha almradi hayahatarishi
usalama. Utawakuta watu wamejipaka masinzi, au rangi za ajabu ajabu
mwilini, kuvaa masoksi usoni, kuvaa mavazi ya kivita na silaha zao na
vikorobwezo vyengine. Baadhi ya sehemu za kazi hufanya mashindano maalum
kuchagua mshindi wa mavazi bora ya siku hii.
Trick-or-Treat
Trick-or-Treat:
Kama tulivyogusia hapo awali kuwa Siku ya Maruhani imekuwa ni siku kuu
ya watoto zaidi kuliko watu wazima. Kwa hivyo, wakati wa jioni watoto
wakiwa wamevalia mavazi yao ya kutisha hupita mitaani, nyumba hadi
nyumba, kubisha hodi na kutoa mzaha wa vitisho (trick) kwa wenye nyumba
iwapo hawatopewa zawadi (treat).
Mara
nyingi hupewa zawadi ambayo zawadi maarufu ni peremendi au vitu
vyengine vitamu. Baadhi ya watu huweka ishara maalum kwenye milango ya
nyumba zao kuashiria kuwa zawadi zimejaa ndani, au huziweka mlangoni
kama chano au tambiko kwa maruhani, na watoto wenye bahati ya kupita
mwanzo hufaidika, na hivyo mwenye nyumba kunusurika na kitisho, au
nyumba yake hunusurika isisibiwe.
Kwa
mujibu wa wanahistoria, inaaminika kuwa huko kale, majini na maruhani
walipokuwa wakiingia mitaani siku hiyo huko Ulaya, watu walioshindwa
kuwababaisha kwa mavazi yao, basi walikuwa wakiwapa zawadi au muhanga
ili wawaachie na wasiwadhuru.
Patry ya Maruhani (Photo: Aaron Favila, AP)
Maparty
nayo hufanyika, yakitawaliwa na michezo ya kuigiza ambayo maudhui zake
kuu ni zile za kutisha, kuadhibu na mauti. Halkadhalika vipindi vya
televisheni na redio pia hutawaliwa na maudhui ya Siku ya Maruhani
zikiwemo nganu na picha za kutisha.
Baadhi
ya watu huitumia vibaya siku hii kwa kufanya vitendo vya kihalifu.
Mpaka wakati tukiingia mitamboni bado hatujapata ripoti kamili ya vyombo
vya usalama nchini Marekani kukhusu matukio ya kihalifu yaliyoripotiwa
hiyo jana. Tuombe salama iwe hakuna mtu yoyote aliyedhurika.
Lakini,
ikiwa hakuna matukio yoyote mabaya yaliyotokea nchini humu, basi
jinamizi la Siku ya Maruhani kwa mwaka huu litakuwa limeikumba Zanzibar.
Kwani kinyume na Marekani na Ulaya ambako maruhani, majini, pepo na
mazimwi hushuka kila mwaka, kwa Zanzibar hushuka kila baada ya miaka
mitano. Na kwa vile hushuka kila baada ya muda huo, basi yakishuka huwa
makali zaidi. Mwaka huu yameshuka yakiwa yamevalia mavazi ya kutisha,
masoksi na masinzi nyusoni na silaha nzito nzito na vimbwanga vyengine
yakibisha hodi milangoni na kusema "trick-or-trick".
Wazanzibari
walikuwa wamezoea kuyapa peremendi, pipi na zawadi nyenginezo iwapo
watashindwa kuvaa mavazi ya kuyababaisha ili yawaachie kuendelea kuishi
angalau katika hali duni. Lakini mwaka huu Wazanzibari wamesema ng'o!
Wamekataa kutoa chano, na kwa hivyo tayari yamevinjari kutaka kuwadhuru.
Sherehe
za hapa na pale zimekuwa zikiripotiwa, na vyombo vya khabari navyo
vimekuwa vikitenga muda maalum kutangaza michezo ya kuigiza na nganu
zenye maneno ya kutisha kama vile "hatutoi", "watarudi" na mengineyo.
No comments:
Post a Comment