Dar es Salaam.
Sherehe 30 za maadhimisho ya kitaifa zinazofanyika nchini kila mwaka huenda ‘zikachinjwa’ kutokana na kasi ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ya kupunguza gharama na kubana matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
Sherehe 30 za maadhimisho ya kitaifa zinazofanyika nchini kila mwaka huenda ‘zikachinjwa’ kutokana na kasi ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ya kupunguza gharama na kubana matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
Wasiwasi wa
kufutwa kwa maadhimisho hayo ya kitaifa umekuja baada ya Rais Magufuli
juzi kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyopangwa
kuadhimishwa Desemba Mosi kabla ya hapo, alifuta sherehe za Uhuru ambazo
zingefanyika Desemba 9.
Rais aliagiza kuwa fedha
zitakazotumika kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, zitumike
kununua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) na zile za
Siku ya Uhuru zitumike kwa usafi wa mazingira ili kupambana na
kipindupindu.
Katika mwendelezo huo, jana Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipiga marufuku utengenezaji na
uchapishaji wa kadi za Krismasi na Mwaka Mpya kwa gharama za Serikali.
Katika
taarifa yake, Balozi Sefue ameelekeza kuwa yeyote anayetaka kutengeneza
au kuchapisha kadi hizo, afanye hivyo kwa gharama zake na ameagiza
fedha zilizopangwa kugharamia utengenezaji na uchapishaji huo, zitumike
kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi za umma zinadaiwa na
wananchi na wazabuni waliotoa huduma kwao au zipelekwe katika matumizi
mengine ya kipaumbele.
Sherehe sasa kwa vipaumbele
Akizungumzia
kufutwa kwa maadhimisho ya sherehe za kitaifa, Sefue alisema Rais
Magufuli amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo kisheria na kuwa
hatua hiyo si endelevu, bali kwa kuangalia vipaumbele.
Sheria
ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35), inampa Rais
mamlaka ya kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko.
Kutokana
na sheria hiyo, ndiyo maana Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alitangaza
Novemba 5 mwaka huu, kuwa ya mapumziko katika kuhitimisha uongozi wa
awamu ya nne na kuukaribisha wa awamu ya tano.
“Maadhimisho
haya yana umuhimu lakini si lazima yafanyike kila mwaka, tunaweza
kuamua mwaka huu tufanye au turuke mwaka mmoja. Siku ya Ukimwi ina
umuhimu na siku ya Uhuru ina umuhimu pia, lakini tunapima kwa kuangalia
wapi kuna mahitaji zaidi,” alisema.
Alisema uamuzi huo
wa Rais ni njia mpya ya kupanga vipaumbele kutokana na hali halisi
ilivyo katika sekta zenye mahitaji makubwa na ya haraka.
Katika
hotuba yake ya kuzindua Bunge ya Novemba 20, Rais Magufuli alisema
Serikali itadhibiti warsha, semina, makongamano na matamasha ambayo
yanatumia fedha nyingi za lakini hayana tija.
Alisema atahakikisha kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
“Tutaziba
mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali
uwezo wake wa kuwahudumia wananchi,” alisema katika hotuba hiyo.
Baadhi
ya maeneo ambayo alisema yatasimamiwa ili kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali ni kufuta safari
za nje, posho za kujikimu na kodi.
Wazungumzia kasi ya Magufuli
Hatua hiyo ya Rais Magufuli, imepongezwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati.
Aliyekuwa
mgombea wa ubunge wa Segerea, Julius Mtatiro alisema Rais alitakiwa
kuandaa utaratibu wa kufuta sherehe hizi kila mwaka ili fedha zitumike
katika sekta nyingine za kimaendeleo.
“Niliposikia
amefuta nilidhani ni kwa miaka yote kumbe ni mwaka huu tu, inawezekana
labda ni kwa sababu Serikali haina fedha na wala si kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima,” alisema.
Alisema sherehe hizo ni
vyema zikafutwa kabisa kwani hazileti maana kutumia fedha nyingi wakati
wanawake wanajifungulia sakafuni na watoto wanaketi chini madarasani.
Meneja
Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu, Godfrey Bonaventure
alipongeza hatua ya Rais Magufuli huku akitaka hatua hiyo iwe endelevu.
“Afanye hivi miaka yote, tumekuwa na utaratibu usiopendeza ambao Serikali inakuwa na matumizi yasiyo ya lazima,” alisema.
Alisema
anachofanya Rais Magufuli ni kutumia kile kidogo kilichopo na
kukiwekeza katika maendeleo badala ya kutumika katika matumizi yasiyo na
tija.
Bonaventure alimtaka pia kufuta sherehe za kupongezana baada ya bajeti kupita na mambo mengine yasiyo na msingi.
“Masuala ya safari, semina, vikao na ‘overtime’ fedha huwa zipo lakini masuala muhimu siku zote tunaambiwa fedha hazitoshi, kwa nini?” alihoji Bonaventure.
No comments:
Post a Comment