Prof. Jay Aanza Kuwapigia Debe Wasanii kwa Rais Magufuli - LEKULE

Breaking

14 Nov 2015

Prof. Jay Aanza Kuwapigia Debe Wasanii kwa Rais Magufuli

MBUNGE mteule wa Mikumi kupita Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Haule aka Profesa Jay, amemtaka Rais John Magufuli kumteua msanii mmoja kuwa mbunge katika nafasi zake 10, ili akawakilishe kundi wasanii bungeni.

Profesa Jay, ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, amesema kuwa Rais anapaswa kufanya hayo kwa vile serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imewatumia wasanii hao katika harakati zake za kuingia madarakani.

Akizunguza na wandishi wa habari nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana, Profesa Jay, amesema kuwa Rais anapaswa kutambua umuhimu wa wasanii hao badala ya kuwatumia katika mambo mbalimbali ya kisiasa kisha kuwatelekeza.

“Wanasiasa wamekuwa wakiwatumia sana wasanii wakati wa kampeni lakini wakimaliza wasanii husahaulika kabisa,” amesema Prof. Jay.

Akizungumzia mpasuko kati ya wasanii ambao walikuwa wakishabikia chama tawala na kuchukia vyama pinzani, amesema hana kinyongo nao kwani kila mtu alikuwa na mapenzi yake lakini anashukuru kuwa wako waliyomuunga mkono japo walikuwa wakishabikia CCM, ambapo aliwatajana majina kuwa ni Mwinjuma Hamisi (Mwana F), na Judith Wambura (Lady Jay Dee).

Prof. Jay, amesema wapo baadhi ya wasanii ambao walidhani kuwa kuingia bungeni ni jambo ambalo haliwezekani kwa msanii hususani kupitia katika chama cha upinzani.

“Mimi nimewasamehe wasanii wote jambo hawakuwa katika upande wake lakini pia nawapongeza wale wote ambao walikuwa na mimi cha msingi sasa tuungane na tufanye kazi,” amesema.

Mbali na hilo Prof. Jay amesema licha ya yeye kuwa mbunge wa jimbo la Mikumi kamwe hawezi kuachana na fani yake ya mziki kwa kuwa fani hiyo ni sehemu ya mafundisho kwa jamii.

Kuhusu kuchaguliwa kwake kuwa mbunge Prof. Jay amesema yeye ni mbunge wa jimbo ambapo anatakiwa kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa wala dini.

“Kwa sasa ninayo kazi moja ya kuhakikisha ninavunja makundi ninajua kwa sasa yapo makundi mengi kutokana na uchaguzi lakini jambo pekee ni kuvunja makundi kwa lengo la kuwapatia maendeleo wananchi,” anasema Prof. Jay.

Prof. Jay amesema hakuna haja ya makundi hayo kuendelea kuwepo, kwani kinachotakiwa hivi sasa ni watu Wanamikumi kutumia fulsa zote kwa ajili ya kujisogezea maendeleo huku wakikumbuka kuwa maendeleo hayana itikadi.


“Sina sababu ya kuendeleza makundi, wana Mikuni walikuwa kama wakiwa katika jimbo lao lakini kwa sasa kinachotakiwa ni kuhakikisha wanapata maendeleo hususani katika sekta ya afya,” alisema Prof. Jay.

No comments: