Polisi yapiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa nchini - LEKULE

Breaking

7 Nov 2015

Polisi yapiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa nchini


Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imepangwa kufanyika kwa nyakati tofauti kwa madai ya kuwepo na hali tete ya  kisiasa.

Akizungumza na wanahabari jijini  Dar es Salaam leo, msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera Bulimba amesema, polisi imefikia hatua hiyo kutokana na hali ya kisiasa ilivyo kwa sasa.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, vyama vya CCM na Chadema tayari vilikuwa vimeshawasilisha maombi ya kufanya mikutano na maandamano sehemu mbalimbali hapa nchini.

Hata hivyo, SSP Bulimba amesema kuwa,  kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na vyombo vya usalama nchini  hali ya kisiasa kwa sasa nchini bado si nzuri kwani bado kuna mihemko mikubwa ya kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu uliomalizika wiki iliyopita.

“Baadhi ya Vyama vya Siasa vimekuwa vikiomba kufanya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima kwa siku moja na vingine maandamano yasiyo na kikomo. Katika hali ya kawaida hili halikubaliki,” amesema SSP Bulimba na kuongeza:

“Tathmini iliyofanywa na vyombo vya usalama imebaini kuwa bado kuna mihemko mikubwa ya kisiasa. Tukiruhusu haya kufanyika kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Bulimba amesisitiza: “Jeshi la Polisi nchini bado linasisitiza katazo lake la awali la mikutano na maandamano hadi hapo hali ya kisiasa itakapotengamaa.”

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwasihi kuendelea na shughuli zao za maendeleo.


Juma lililopita Chadema kilipanga kufanya maandamano nchini nzima kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu hususani ngazi ya Urais, lakini maandamano hayo yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi

No comments: