Jeshi
la Polisi mkoani Katavi limefanikiwa kuzuia kufungwa kwa ndoa
iliyohusisha watoto, muolewaji akiwa na umri wa miaka 14 na muoaji ana
umri wa miaka 17.
Kwa
mujibu wa taarifa, bibi harusi ni mwanafunzi wa darasa la nne katika
Shule ya Msingi Mwamkulu iliyopo kijiji cha Senta John Mwamkulu,
Wilayani Mpanda, mkoani Katavi, na bwana harusi aliacha shule alipokuwa
darasa la tatu. Mwanafunzi huyo (14), (jina linahifadhiwa) siku ya
harusi alikuwa afanye mtihani wa wilaya, lakini alikutwa akiwa amevaa
shela tayari kwa kufungishwa ndoa ya kimila nyumbani kwao kwa mahari ya
ng’ombe kumi na moja.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo
lilitokea juzi saa saba mchana katika kijiji Senta John Mwamkulu, wilaya
ya Mpanda.
Alisema
polisi wakiwa na viongozi wa elimu wa Manispaa ya Mpanda, walienda
nyumbani kwao na kukuta msichana huyo akiwa na shela tayari kufungishwa
ndoa kinyume cha sheria.
Alisema
jeshi hilo linamshikilia bwana harusi (jina linahifadhiwa), baba yake
bwana harusi Ntunga Mkubaneja (40) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Mwankulu, Raphel Kweka, anayedaiwa kupewa Sh500,000 ili afute jina la
mwanafunzi huyo shuleni.
Akisimulia
tukio hilo, Kamanda Kidavashari alisema wakati mchakato wa kufungwa kwa
ndoa hiyo ukiendelea, mkazi wa kijiji hicho alifunga safari mpaka
ofisini kwake na kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa ndoa hiyo kinyume cha
sheria.
“Tulipewa
taarifa kuwa kuna mwanafunzi anaozeshwa kinyume cha sheria na harusi
yake inafungwa mchana wa tarehe tisa, mwezi huu. Tulijiandaa
tukakubaliana na watu wa elimu kisha tukaenda kijijini na kukutana na
shamra shamra za kumuozesha mwanafunzi kama tulivyoambiwa,”alisema.
Ofisa
Elimu wa Manispaa ya Mpanda, Vincent Kayombo alisema mwanafunzi huyo
alikuwa darasa la nne na kuwa siku ya harusi yake alitakiwa kufanya
mtihani wa wilaya (Mock).
Kayombo
alisema alishangazwa na hatua ya wazazi kuamua kumuozesha mtoto wao
wakati akiwa bado darasa la nne, kwa mahali ya ng’ombe 11 kinyume cha
sheria.
Alilitaka
Jeshi la Polisi kufanya utafiti juu ya tuhuma za mwalimu mkuu kuhusika
kwenye sakata hilo, kwa kudaiwa kupokea fedha ili akibainika, hatua za
kisheria zichukuliwe dhidi yake.
“Mleta
taarifa alimtaja mwalimu mkuu kuwa alipewa fedha kuhalalisha mwanafunzi
huyu aolewe, kwa kuwa wapo chini ya vyombo vya sheria haki
itatendeka,”alisema Kayombo.
Naye
Ofisa Maendeleo wa Manispaa ya Mpanda, Zena Kapama aliviomba vyombo vya
sheria kuchukua hatua dhidi ya jambo hilo ili kukomesha vitendo vya
kuozesha wanafunzi wakiwa kwenye umri mdogo.
“Tulimkuta
mtoto akiwa amevaa shela tayari kuolewa, alikiri kuwa haikuwa ridhaa
yake kuolewa na ndipo tukafanikiwa kuwakamata bwana harusi, bibi harusi
mwenyewe, baba wa bwana harusi na mama yake bwana harusi huku baba mzazi
wa bwana harusi akikimbia,”alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari msichana huyo aliyenusurika kuolewa, alisema haikuwa ridhaa yake kuolewa na kijana hiyo.
“Baba
alilazimisha niolewe akidai kuwa shuleni sina akili, nilikataa nikaomba
niendelee kusoma shule kwa sababu elimu itanisaidia nikiwa mkubwa
lakini alikataa. Niliomba niende mjini kuishi kwa baba mkubwa, yote baba
alikataa alichotaka yeye niolewe,” alisema.
Alisema
suala lake la kuolewa lilileta mzozo nyumbani kwao kwa kuwa mama yake
hakuwa tayari mwanaye huyo aolewe akiwa na umri mdogo.
Mama
wa mwanafunzi huyo, Esther Martin alisema binti yake alilazimishwa
kuolewa na kwamba hakuwa na uwezo wa kukataa kwa kuwa tayati mumewe
alikuwa amepokea mahali ya ng’ombe 11.
“Mtoto
aliitwa mbele yangu kulazimishwa aolewe kwa madai hana akili shuleni
kwa kuwa hajui kusoma, alilazimika kukubali tu nilimshauri baba yake
asimuozeshe kwa sababu hata Serikali haitaki, akakataa,”alisema mama
huyo.
Baba wa bwana harusi huyo, Mkubaneja alisema alilipa mahali ili mwanaye amuoe msichana huyo bila kujua kama alikuwa mwanafunzi.
Kwa
upande wake bwana harusi, ambaye alidai kuishia darasa la tatu alisema
aliamua kumuoa msichana huyo baada ya kumpenda, lakini hakujua kama ni
mwanafunzi baada ya wazazi wa binti huyo kukubali kupokea mahali toka
kwa wazazi wake.
Mwalimu
Mkuu Kweka, alikataa kuhusika kumuozesha mwanafunzi huyo, pia
alikanusha madai ya kupokea fedha kutoka kwa baba wa binti huyo.
Alisema
taarifa zote za mwanafunzi huyo ambaye alitakiwa kufanya mtihani wa
darasa la nne siku ya harusi yake ikiwamo namba yake ya mtihani zipo.
“Vielelezo
vyote ambavyo vinamuhusu mwanafunzi vipo likiwamo daftari la
mahudhurio, ninachojua huyu binti ni mtoro wa ‘rejareja’. Sijawahi
kuchukua kiasi chochote cha hela kwa mzazi wake, wala ndugu yake wala
mtu yeyote anayefanana naye,” alisema Mwalimu huyo.
Mtetezi
wa masuala ya kijinsia nchini, Gemma Akilimali alilitaka jeshi la
polisi kuhakikisha wahusika wanapelekwa mahakamani, ili sheria ichukue
mkondo wake.
“Tuwashukuru
waliojitahidi kumuokoa mtoto huyo kabla hajaolewa, ombi letu
wanaharakati ni kwamba kesi hiyo isiishie hewani, wazazi waliopokea na
kutoa mahali lazima wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe
fundisho,”alisema.
Alisema
ikiwa jamii itaendelea kutoa ushirikiano kwa kufichua wazazi wenye
tabia ya kuozesha wasichana wenye umri mdogo, tatizo hilo litapungua.
Akilimali aliongeza kuwa mwanafunzi huyo anatakiwa kurejea shuleni ili aendelee na masomo yake.
No comments:
Post a Comment