15 Nov 2015

Manufaa mengi ya mende kwa binadamu


Mende wana manufaa mengi sana kwa binadamu

Mende huchukiwa sana na watu na huhusishwa na uchafu na maradhi. Lakini wajua kwamba wadudu hawa wana manufaa makubwa sana kwa binadamu?
Mjini Havana, nchini Cuba kuna aina ya mende ambao hufugwa kama wanyama vipenzi na hata visa vyao husimuliwa kwenye hadithi, anasimulia Mary Colwell.
Kwenye kisa kimoja, mende kwa jina Martina huwafanyisha mtihani wanaotaka kumchumbia kwa kuwaudhi kila wanapomtembelea.
"Mwaga kahawa kwenye viatu vyao uone watalichukulia vipi hilo,” anapendekeza nyanyake Martina. "Ni muhimu sana kujua mumeo mtarajiwa hufanya nini anapokasirika – mtihani wa kahawa hufanikiwa.”
Kuna aina 4,500 ya mende, na ni aina nne pekee ambao huwa waharibifu.
Wengi hawaishi karibu na nyumba za watu na hutekeleza jukumu muhimu katika ikolojia kwa kula vitu vilivyokufa na vinavyooza.

Baadhi ya mende huishi pamoja na kusaidiana
Baadhi wana sifa nzuri na huishi pamoja na kusaidiana katika kutafuta chakula na makazi. Wana uwezo wa kuishi katika mazingira magumu. Aina moja kwa jina Eublaberus posticus wanaweza kuishi mwaka mmoja kwa kunywa maji pekee.
Wale wazito zaidi, huwa na uzani wa gramu 35, na urefu wa sentimeta 8 na huishi Australia. Wale wadogo zaidi huishi Ulaya na Amerika Kaskazini na wana urefu wa sentimeta moja pekee.
Badala ya kuwachukia, wanasayansi huwafurahia sana na kuwatumia kwa manufaa ya binadamu. Mwaka 1999, mende walitumiwa na Prof Robert Full katika Chuo Kikuu cha California, Berkley, kumpa wazo la kuunda roboti ya miguu sita iliyosonga upesi na kwa urahisi.
Mende huwa thabiti sana, na wakianguka huwa wanainuka upesi na kwa urahisi kwa kutumia mabawa.
Miguu ya mende pia imekuwa ikitumiwa na wavumbuzi wanaotengeneza miguu bandia ya kutumiwa na binadamu.
Kuna pia mende ambao wamekuwa wakiunganishwa na kompyuta ndogo inayowekwa mgongoni na kuongozwa kufika maeneo ambayo mwanadamu hawezi kufika.


"Nilipoona hili mara ya kwanza, nilishangaa sana,” mtafiti mkuu katika mradi huo unaoendeshwa katika Chuo Kikuu cha A&M cha Texas, Hong Liang anasema.
Mende wanatumiwa pia katika matibabu. Wanasayansi kwa miaka mingi wamekuwa wakishangazwa na uwezo wa mende kukaa muda mrefu maeneo yenye sumu na uchafu bila kudhurika. Wamegundua kwamba huwa wanatoa kemikali za kupigana na sumu.
Wanaweza kusaidia katika kutengeneza dawa za kusaidia binadamu kukabiliana na bakteria zinazohangaisha sana watu kwa mfano E. Coli na MRSA ambazo zimekuwa hazisikii dawa.
Hii si mara ya kwanza mende kutumiwa kwa sababu za kimatibabu. Mwanahabari Lafcadio Hearn karne ya 19 alipitia maeneo ya kusini mwa Marekani na kuripoti jinsi watu wenye pepopunda walivyokuwa wakipewa chai iliyotengenezwa kwa kutumia mende.
“Sijui ni mende wangapi hutumiwa hadi upate kikombe cha chai, lakini wakazi wa New Orleans wana imani sana na tiba hii,” aliandika.
Leo katika hospitali Uchina, krimu inayotengenezwa kwa kutumia ungaunga wa mende waliosiagwa hutumiwa kutibu vidonda vya moto na pia humezwa kutibu vidonda vya tumbo.
Mende wanahitajika sana hivi kwamba Wang Fuming aliamua kufungua biashara ya ufugaji mende eneo la Shandong, mashariki mwa Uchina. Huwa anafuga mende 22 milioni kwa wakati mmoja. Anasema tangu 2010, bei ya mende waliokaushwa imepanda mara kumi.

Mende hupikwa na kuliwa nchini Uchina
Mende pia huliwa Uchina!

No comments:

Post a Comment