Masaju aapishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) - LEKULE

Breaking

6 Nov 2015

Masaju aapishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)



Rais Dk John Magufuli amemuapisha George Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla fupi iliyofanyika leo Ikulu mjini Dar es Salaam.


Huo ni uteuzi wa kwanza kufanywa na Rais Dk Magufuli tangu aapishwe jana katika sherehe zilizofana na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake wakiwemo marais takribani wanane toka nchi kadhaa za kiafrika.
  
Kwa uteuzi huo, Masaju anaendelea kuhudumu katika nafasi hiyo aliyoishikilia tangu Januari 5 mwaka huu baada ya kuteuliwa na kisha kuapishwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Fredrick Werema aliyejiuzulu.
  
Jaji Werema alijiuzulu nafasi hiyo Desemba 2014 kutokana na kashfa ya  uchotaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta escrow ya Benki Kuu.  Aliishikilia nafasi hiyo tangu Oktoba 20, 2009.
  
Hata hivyo, Werema amekuwa akikana kuhusika moja kwa moja katika kashfa hiyo na kusisitiza kuwa ushauri wake kuhusu suala hilo haukueleweka vizuri.
  
Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa, Masaju ameahidi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa pindi masuala ya kisheria yanayohitaji utendaji wa kiweledi toka kwenye ofisi yake yatakapojitokeza.
  
“Pia, niwashukuru Watanzania kwa utulivu na utii wa sheria waliouonyesha wakati wote wa mchakato wa uchaguzi uliopelekea kudumu kwa amani na utulivu wetu” amesema Masaju.
  
Kabla ya kujiunga na ofisi ya Mwanasheria Mkuu kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo mwaka 2009, Masaju alifanyakazi kama mshauri wa rais katika masuala ya kisheria.
Masaju pia anafanyakazi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sheria Tanzania.


Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju akila kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli mara baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam

Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akitia saini hati ya kiapo mara baada ya kumuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akimkabidhi nyaraka Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju mara baada ya kumuapisha Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan (kushoto) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Jaji Mkuu Othuman Chande,Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan na spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anne Makinda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na wanafamilia ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments: