Uamuzi
wa Rais Dk. John Magufuli kueleza kwa kina namna safari holela za nje
ya nchi zinavyoligharimu taifa mabilioni ya fedha, umeianika wazi
Serikali iliyopita ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na
kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya
siasa nchini.
Wachambuzi
mbalimbali wa masuala ya kiasiasa wanasema kuwa ujasiri wa Rais
Magufuli kueleza bila kificho jinsi safari za nje zinavyogharimu taifa
kabla ya kutangaza msimamo mkali wa kuzidhibiti umedhihirisha pasi na
shaka kuwa rais huyo mpya amedhamiria kubana matumizi holela ya fedha za
serikali na badala yake kuzielekeza katika shughuli za maendeleo kwa
nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Wakati
akilihutubia Bunge la 11 Ijumaa iliyopita kisha kulizindua rasmi, Rais
Magufuli aliwataka wabunge na Watanzania wote wamuunge mkono katika
uamuzi wake wa kupiga marufuku safari holela za nje huku akisisitiza
kuwa kwa kufanya hivyo, fedha nyingi zinazopotea zinaweza kutumiwa
katika kuboresha huduma za jamii.
Akitaja
kwa mifano jinsi safari hizo za vigogo nje ya nchi zinavyoligharimu
taifa, Magufuli alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015
peke yake, taifa lilitumia Sh. bilioni 356.324 kugharimia safari hizo;
kiasi ambacho kwa maelezo yake, kingetosha kujenga barabara ya lami ya
urefu wa kilomita 400 na pia kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo
ikiwamo ya maji, elimu na afya.
Alisema
mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa ni tiketi za ndege (Air
ticket) Sh. bilioni 183.160, mafunzo nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na
posho za kujikimu (Per Diem Foreign) Sh. bilioni 104.552.
Magufuli
alizitaja wizara na taasisi za umma zilizoongoza kwa kutumia fedha
nyingi kwa ajili ya safari za nje ya nchi kuwa ni Bunge, Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara
ya Mambo ya Ndani.
Kwa
mujibu wa Rais Magufuli, sasa safari hizo ni marufuku na pale
inapolazimu, ni lazima kibali kitoke kwake au kwa Katibu Mkuu Kiongozi
Ikulu, na kwamba, kuanzia sasa watakaokuwa wakijumuishwa kwenye misafara
ya lazima nje ya nchi ni watu muhimu tu wanaohitajika katika safari
husika.
“Hizi
fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha
ya chini, kama afya, maji, elimu na umeme. Mfano, fedha hizi zingetosha
kutengeneza kilomita 400 za barabara za lami. Tujiulize, zingeweza
kutengeneza zahanati ngapi? nyumba za walimu ngapi? Madawati mangapi?” alihoji Rais Magufuli wakati akielezea suala hilo bungeni na kuongeza:
“Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.”
Alivyo "Ivua Nguo" Serikali ya Awamu ya nne
Hotuba
ya Rais Magufuli aliyoitoa mwishoni mwa wiki inaonyesha wazi kuwa
misafara ya mara kwa mara ya viongozi mbalimbali kwenda nje ya nchi
ilikuwa ikiligharimu taifa kwa kiasi kikubwa kwani fedha hizo zingefanya
mambo mengi kwa manufaa ya nchi badala ya kunufaisha vigogo wachache.
Wakati
fedha nyingi zikitumika kwa safari hizo, bado hali ni mbaya katika
utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii; mambo ambayo Magufuli
amesisitiza kuwa kamwe hatakubali kuyaruhusu katika serikali yake ya
awamu ya tano.
Fedha
hizi zilizotafunwa na viongozi mbalimbali kupitia safari za nje (Sh.
bilioni 356) zingeweza kufanikisha mambo mengi ya maendeleo kwa taifa
kama ifuatavyo.
1. Madawati 3,098,469
Bei
ya dawati moja linalochukua wanafunzi watatu wa shule za msingi huwa ni
kati ya Sh. 80,000 hadi 150,000, wastani wake ukiwa ni Sh. 115,000.
Kwa
sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotumika kwa safari za vigogo (Sh. bilioni
356) zingetumika kununua madawati, maana yake yangepatikana madawati
3,098,469 na hivyo kumaliza tatizo hilo katika shule za msingi nchini.
2. Visima vya maji safi 35,632
Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali, gharama za kuchimba kisima cha maji safi
huwa ni kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 kwa kina cha mita moja,
kutegemeana na jiografia ya eneo husika.
Kwa
sababu hiyo, kama kisima kitakuwa na urefu wa mita 100 na kitachimbwa
kwa Sh. 100,000 kwa kila mita moja, maana yake kiasi cha fedha
kitakachohitajika ni Sh. milioni 10.
Hivyo,
ikiwa fedha za safari za nje (Sh. bilioni 356) zingetumika kuchimba
visima vya maji safi vya thamani hiyo, maana yake vingepatikana visima
35,632. Visima hivyo vingegawanywa sawa katika wilaya 133 nchini, maana
yake kila wilaya ingepata mgawo wa visima 268.
3.Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu
Mwanafunzi
wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh.
4,219,500 kwa mwaka. Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni
Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh.
620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.
Kwa
sababu hiyo, ikiwa fedha za safari za nje alizozitaja Rais Magufuli
zingetumika kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa
kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia 100, maana
yake wanufaika kwa mwaka wangekuwa wanafunzi 84,447.
4.Magari ya kubebea wagonjwa
Mwaka
jana, Agosti 28, kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa
gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa
Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milion 76.
Kwa
sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotajwa na Rais Magufuli kuwa zilitumika
kusafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika kununua magari ya
wagonjwa kama walilopata msaada Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, maana
yake taifa lingepata magari mapya ya wagonjwa 4,688.
5.Zahanati 4,454.
Septemba
16 mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba,
alisema kuwa katika jimbo lake, wamekamilisha ujenzi wa zahanati za
vijiji kadhaa kwa wastani wa Sh. milioni 80 kwa kila moja.
Kwa
sababu hiyo, kama fedha za safari alizozitaja Rais Magufuli kuwa
zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi (Sh. bilioni 356) zingetumika
kujengea zahanati kama za jimbo la Bumbuli, maana yake taifa lingepata
zahanati mpya takriban 4,454.
6.Maabara shule za Sekondari 6,122
Mkuu
wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi kukaririwa
Aprili 20, 2015, akisema kuwa shuleni kwake walikamilisha ujenzi wa
maabara mojawapo kwa Sh. milioni 58.2.
Kwa
sababu hiyo, kama fedha za safari kusafirisha vigogo nje ya nchi wakati
wa Rais Kikwete mwaka juzi na mwaka jana zilizotajwa na Magufuli (Sh.
bilioni 356) zingetumika kujenga maabara za shule za sekondari kama
Sekondari ya Tandika, maana yake zingejengwa maabara 6,122 na kumaliza
tatizo hilo nchini.
7.Mikopo kwa wajasiriamali( Kila mmoja 500,000)
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali wanawake ni ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Hata
hivyo, kama ingetokea serikali ya Rais Kikwete ingesitisha matumizi ya
fedha za safari za nje kwa viongozi alizozitaja Rais Magufuli (Sh.
bilioni 356) na badala yake kuzielekeza katika kuwakopesha mitaji
wajasiriamali wanawake kwa kiasi cha Sh. 500,000 kila mmoja, maana yake
wanufaika wangekuwa ni kina mama 712,648.
8.Bodaboda aina ya Boxer
Bei ya juu ya pikipiki aina ya Boxer zinazotumika kwa biashara ya bodaboda ni Sh. milioni 2.5.
Kwa
sababu hiyo, ikiwa fedha za posho za safari alizozitaja Magufuli kuwa
zilitumika katika miaka ya fedha ya 2013/2014 na 2014/2015 (Sh. bilioni
356) kwa ajili ya safari za vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika
kununulia pikipiki hizi kwa ajili ya kuwakopesha vijana wanaotoa huduma
ya usafiri wa bodaboda, maana yake zingepatikana pikipiki za aina hiyo
takriban 142,530.
9.Vipimo CT-Scan 356
Vyanzo
mbalimbali vinaeleza kuwa mashine za kipimo maarufu cha CT-Scan, aina
ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja.
Hivyo,
kama Sh. bilioni 356.324 alizozitaja Rais Magufuli kuwa zilisafirisha
vigogo nje ya nchi zingeelekezwa kununua vipimo hivyo, maana yake
zingepatikana CT-Scan 356 za thamani ya Sh. bilioni moja kila moja na
kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na nyingine nyingi
zikaelekezwa katika hospitali za wilaya na pia vituo vya afya.
10.Daladala Toyota Coaster 6,089.
Kwa
mujibu wa mtandao wa Trade Car View, bei ya kununua gari aina ya Toyota
Coaster iliyotumika lakini iliyo katika hali nzuri ni dola za Marekani
27,896, sawa na takriban Sh. 58,513,255.
Kama
fedha zilizosafirisha vigogo nje ya nchi katika miaka ya fedha ya
mwisho ya Rais Kikwete (Sh. bilioni 356) zingetumika kununulia gari hizi
kwa ajili ya kuwapatia wajasirimali wanaotoa huduma ya usafiri wa
daladala nchini, maana yake zingepatikana daladala 6,089.
No comments:
Post a Comment