Aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana hakuhudhuria
mkutano wa kampeni za ubunge mjini Arusha kwa maelezo kuwa anajiandaa
kutoa tamko kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar.
Maelfu
ya wafuasi wa Chadema jana walifurika kwenye Uwanja wa Ngarenaro mjini
Arusha kuhudhuria kampeni za ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini ambao
uliahirishwa kutokana na kifo cha mgombea kutoka chama cha ACT
Wazalendo, lakini wakakumbana na tangazo kuwa Lowassa hataweza kuhutubia
na badala yake atakuja siku ya kufunga kampeni hizo.
Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, James Mbatia(NCCR- Mageuzi) naye alisema kuwa Lowassa
yupo katika maandalizi ya kikao cha leo kutangaza hatma ya uchaguzi mkuu
uliopita.
“Tulikuwa
tumepanga Lowassa aje katika mkutano huu, lakini kutokana na kufanya
maandalizi muhimu ya mkutano na waandishi wa habari kesho saa 5:00
asubuhi, ameshindwa kuja” alisema James Mbatia, mwenyekiti mwenza wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vinne vya
Chadema, CUF, NLD na NCCR Mageuzi.
“Lowassa atakuja siku ya kufunga kampeni za ubunge katika Jimbo la Arusha hivyo tunaomba radhi,” alisema Mbatia, ambaye pia ni mbunge mteule wa Jimbo la Vunjo na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Lowassa,
ambaye juzi alikuwa na mazungumzo ya saa moja na nusu na mgombea urais
wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif, anatarajiwa kutoa tamko kuhusu hali ya
kisiasa visiwani humo ambayo imekuwa tete baada ya Tume ya Uchaguzi
(ZEC) kufuta matokeo.
“Mheshimiwa anaandaa mambo muhimu atakayozungumza kesho,” alisema Aboubakar Liongo, msaidizi wa Lowassa alipoulizwa kuhusu waziri huyo mkuu wa zamani jana mchana.
Liongo
alisema, mbali na suala la Zanzibar, Lowassa pia ataeleza msimamo wake
kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, ambao yeye na chama chake
cha Chadema wanaamini kuwa matokeo ya kura za urais yaliyokuwa
yanatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni tofauti na waliyokuwa
nayo.
Tayari
Lowassa ameshaeleza kuwa kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka huu ni mwanzo
wa awamu ya pili ya safari yake ya kuelekea Ikulu, akiwataka
wanaomuunga mkono kutokata tama.
“Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini huwezi kuiondoa,” alisema Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07.
Kwenye
mkutano wa kampeni mjini Arusha, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara,
Profesa Abdalah Safari alisema Lowassa pia atazungumzia tamko la polisi
la kuzuia mikutano ya Ukawa na maandamano licha ya kuwa hiyo ni haki
yao.
No comments:
Post a Comment