Mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA Edward Lowassa Jana alitoa shilingi milioni mbili kwa wahanga waliookolewa katika mgodi wa Nyangalata wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga.
Akikabidhi fedha hizo kwa wahanga hao, Lowassa alisema
ametoa fedha hizo kama msaada ili ziwasaidie kwa matibabu kwa muda wote
watakapokuwa hospitalini hapo, ambapo kila mmoja amepatiwa shilingi
laki tano.
Mmoja wa wahanga hao, Joseph Burule alisema
kitendo cha Lowassa kuwatembelea hospitalini hapo kimewapa faraja
kubwa, kwani tangu waokolewe na kuanza kupatiwa matibabu hakuna kiongozi
mkubwa aliyefika kuwajulia hali pamoja na kuwapa pole.
Burule alisema
kitendo hicho kinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi pindi
linapotokea jambo la kusikitisha kama hilo, na kusema kuwa fedha hizo
zitawasaidia kujikimu hospitalini hapo.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga kupitia CHADEMA Salome Makamba aliwaambia wananchi waliojitoza kumsabahi Lowassa kuwa, Lowassa amekuja kuwapa pole wahanga hao na hakuja kwa masuala ya kisiasa.
Novemba 15, 2015 wahanga 5 kati ya 6 waliofukiwa na kifusi katika machimbo ya nyangalata wilayani kahama waliokolewa wakiwa hai baada ya kukaa ndani ya mashimo kwa siku 41, ambapo juzi mmoja kati yao alifariki dunia.
Ni
hivi karibuni baada ya kuokolewa mmoja wa wahanga hao alikaririwa
akimuulizia Lowassa kama alishinda urais wa Tanzania kwenye uchaguzi na
baada ya kuambiwa hakushinda alikosa raha.
No comments:
Post a Comment