Kesi ya Ubunge wa David Kafulila Yaahirishwa Hadi Jumatatu Novemba 30 Baada ya Mlalamikiwa Kutofika Mahakamani - LEKULE

Breaking

27 Nov 2015

Kesi ya Ubunge wa David Kafulila Yaahirishwa Hadi Jumatatu Novemba 30 Baada ya Mlalamikiwa Kutofika Mahakamani



Kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, kupinga matokeo ya ubunge yaliyomtangaza mshindi Husna Mwilima, katika jimbo hilo, imeahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu.
 
Kesi hiyo ipo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, John Utamwa.

Jaji Utamwa alisema mlalamikiwa (Mwilima), katika madai hayo, hakupelekewa wito wa mahakama, hivyo anaamuru wito utolewe ili mlalamikaji aende mahakamani kujibu madai hayo ambayo anatetewa na mwanasheria wa serikali, Juma Masanja.

Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa mlalamikaji, Daniel Rumenyela, alidai mlalamikiwa (Mwilima), hakupatikana kwa ajili ya kuitwa shaurini hata akipigiwa simu hapokei.
 
“Kutokana na mlalamikiwa wa kwanza kutopatikana, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora inatoa siku tatu hadi Novemba 30, mwaka huu, (Jumatatu), ajibu madai hayo,” alisema Rumenyela. 
 
Kesi hiyo namba 2 ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo, pia ina washtakiwa wengine ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hii ndogo ya awali kabla ya kesi ya msingi, Mahakama itaamua gharama ambazo Kafulila atatakiwa kulipa kama gharama za dhamana ambayo kisheria kwa washtakiwa watatu haizidi Sh. milioni 15.

Katika kesi ya msingi, Kafulila anaomba Mahakama imtangaze mgombea aliyepata kura nyingi kwani aliyetangazwa siye mbunge halali kutokana na kupata kura chache.


Katika shauri hilo, Kafulila alimtaja Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mrisho Gambo, kama wahusika waliofikisha ujumbe huo toka juu Oktoba 28, mwaka huu, saa 8:00 mchana kwa Msimamizi wa Uchaguzi kushinikiza matokeo batili kutangazwa.

No comments: