NA BASHIR YAKUB.
NILIWAHI
kueleza namna ya kuanzisha kampuni pamoja na usajili wa jina
la biashara. Katika makala hayo pia nilieleza tofauti kati ya
kusajili kampuni na kusajili jina la biashara.
Hii
ilikwenda sambamba na maelezo ya tofauti za kiuchumi ya vyote
viwili. Ifahamike kuwa hizi zote ni njia za kisasa za
kujitafutia kipato. Makala ya leo yanaeleza namna ya kisheria
ya kuanzisha SACCOS.
Tutaona
utaratibu mzima ambao unaweza kupitia katika kulifanikisha
hili. Muhimu ni kujua kuwa SACCOS nayo ni njia kati ya njia
za kisasa za kujipatia na kujiongezea kipato. Aidha utaratibu
mzima wa kuanzisha na kuendesha SACCOS unaongozwa na Sheria
namba 6 ya 2013 ya vyama vya ushirika ambayo ndiyo msingi wa
makala haya.
1.SACCOS NI NINI ?
SACCOS
ni kifupi cha neno la kiingereza lijukanalo kama Saving And
Credit CO-operative Society. Kwa Kiswahili kizuri ni chama cha
ushirika cha akiba na mikopo.
Kwa
faida tu ni kuwa, kwa mara ya kwanza SACCOS zilianzishwa
Ujerumani na mtu aitwaye Fredrick Taylor. Sura ya SACCOS
aliyoanzisha Taylor imekuwa ikibadilika kadri shughuli za
kijamii na kiuchumi zinavyokua mpaka kufikia aina ya SACCOS
zilizopo sasa.
2. SACCOS KIUCHUMI.
Saccos
ni asasi ya kifedha. Ni muungano wa watu ambao lengo lao ni
kukusanya fedha na kukopeshana au kufanya biashara moja kwa
moja na kugawana faida. Taratibu za kukopeshana na kufanya
biashara katika Saccos hufanywa na watu wenye msimamo au
fungamano linalofanana.
Hii
ina maana wanaweza kuwa watu wanaofanya kazi ya aina moja kwa
mfano walimu, wafanyabiashara, wafanyakazi katika ofisi fulani,
vijana wanaoishi eneo moja mtaani, wanawake walio katika eneo
moja, waumini wanaosali katika msikiti au kanisa moja,
wakulima,wavuvi, wafugaji, wanakijiji na watu wote wa aina hiyo.
Watu walio katika mafungamano ya aina hiyo ndio wanaweza kuunda
Saccos.
3. LENGO KUU LA SACCOS.
Lengo
kuu la Saccos ni kuwa, ni ushirika ambao lengo lake ni
kuondoa umasikini na kuinua uchumi wa wanachama na jamii kwa
ujumla. Hii ndio sababu kubwa ya kuanzisha Saccos. Ni kukuza
kipato kwa manufaa ya kiuchumi .Ni biashara ya kuongeza kipato
kama zilivyo biashara nyingine za uanzishaji wa makampuni n.k.
4. MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZISHA SACCOS.
Kwanza
kabisa ni uwepo wa hiari ya kila mwanachama. Ni kosa
kumshurutisha mtu kuingia katika Saccos. Ni lazima kila
anayeingia afanye hivyo kwa hiari yake. Pili ni muhimu
wanaoanzisha Saccos wakawa na matatizo ya aina moja. Kama
tatizo ni ajira na Saccos inaundwa ili kukabiliana na hilo
basi yapasa hilo ndio liwe tatizo la wanachama wote n.k. Kwa
ufupi wanachama wawe ni watu wanaoshiriki (share) tatizo.
5. TARATIBU RASMI ZA KUANZISHA SACCOS.
( a )
Kwanza kabisa hakikisha hampungui watu watano. Yaani muwe watu
watano na kuendelea. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 38(1)
cha sheria ya vyama vya ushirika. Hata hivyo idadi hii ni
kwa waanzishaji wa awali. Hii ni kwakuwa idadi hasa inayotakiwa
ni kuanzia watu ishirini. Msajili wa vyama vya ushirika
atawapa maelekezo ya idadi kwa namna anavyoona kikundi chenu.
( b )
Baada ya idadi hiyo kutimia mtamfuata msajili wa vyama vya
ushirika ambaye hupatikana katika kila makao makuu ya wilaya
mliyopo. Nenda makao makuu ya wilaya na uliza hapo utampata.
Baada ya kusikiliza maelezo yenu msajili ataandaa mkutao ambao
huitwa mkutano mkuu wa uanzishaji ambao msajili mwenyewe ndio
atakuwa mwenyekiti wake. Katika mkutano huo itateuliwa kamati ya
muda ya uanzishaji ambayo itakuwa na wajumbe 5 – 9 akiwemo
katibu, mwekahazina, mwenyekiti na wajumbe wengine.
( c )
Baada ya kamati ya uanzishaji kuundwa itakuwa na kazi ya
kushirikiana na afisa ushirika kuandaa katiba za chama,
sera,miongozo, miradi ya kiuchumi, taratibu za viingilio na
taratibu zote za uanzishaji na uendeshaji.
( d )
Baada ya kazi hiyo kukamilika basi maombi rasmi ya kuomba
kusajiliwa yatawasilishwa kwa huyo afisa ushirika wa wilaya
yakiambatana na nakala nne za sera za chama, kidadisi uchumi,
makadirio ya mapato na matumizi, mikhutasari ya mikutano miwili,
na ada kama itakavyoelekezwa na afisa ushirika.
Tutaeleza
katika makala nyingine umuhimu wa SACCOS, tofauti za kiuchumi
kati ya SACCOS na kampuni na kipi bora kati ya kuanzisha
SACCOS na kampuni.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment