Wakati saa 48 zilizotolewa na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar zikiwa zimemalizika, Ikulu ya Jamhuri ya Muungano imesema haijapokea maombi ya Maalim Seif kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete.
Ijumaa
iliyopita, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari visiwani Zanzibar
kuwa baada ya ZEC kufuta uchaguzi Jumanne iliyopita, alifanya jitihada
kadhaa za kuwasiliana na Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohamed Shein, ili kuzungumzia suala hilo kwa maslahi ya Zanzibar lakini
wito wake huo umekuwa ukipuuzwa.
Maalim
Seif alisema tangu kufutwa kwa uchaguzi, amefanya juhudi za kutafuta
ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wenzake wa kitaifa
akiwamo Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein,
lakini wote wamekuwa wakimkwepa, licha ya kuanza kuwatafuta kwa kutumia
mawasiliano ya simu na ujumbe kupitia wasaidizi wao, akitaka wakutane.
Hata
hivyo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa
kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa Ikulu
imesikitishwa na madai ya Maalim Seif, ikieleza kuwa siyo kweli.
Badala
yake, Ikulu imesema haijapokea ombi lolote kutoka kwa Maalim Seif la
kutaka kukutana na Rais Kikwete tangu siku ya kupiga kura na hata baada
ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi wa Zanzibar.
Taarifa
hiyo ya Ikulu imesema kile ambacho Rais Kikwete amekipokea ni
malalamiko ya CUF kuhusu baadhi ya vitendo kutoka kwa baadhi ya askari
wa Jeshi la Polisi Zanzibar na ombi kwa ajili ya kuwezesha mazungumzo
kati ya Maalim Seif na Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Davis
Mwamunyange.
“Baada
ya hapo, Rais Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, amemuagiza
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuchunguza madai haya
ya CUF na kumletea taarifa. Kadhalika, ametoa maelekezo ofisini kwake ya
kuwezesha mazungumzo kati ya Jenerali Mwamunyange na maafisa wa CUF,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo iliongeza kuwa Rais Kikwete amekuwa akiguswa na hali ya kisiasa na
usalama wa Zanzibar kama ilivyo kwa Watanzania wengine na amekuwa
akifanya kazi bila kuchoka huku akipata ushauri wa kina juu ya
kilichotokea Zanzibar siku chache zilizopita na kupata ufumbuzi.
Taarifa
hiyo ilifafanua zaidi kuwa wakati jambo hilo likiwa bado katika mikono
ya ZEC ambacho ni chombo huru cha uchaguzi, Rais Kikwete yuko tayari
kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wake ili kupata suluhisho jema
kuhusiana na hali ya Zanzibar.
Uchaguzi Kufutwa
Suala la kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar linadaiwa kuviingiza visiwa hivyo katika mgogoro wa kikatiba na kisheria.
Mwenyekiti
wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitaja sababu tisa za kufikia uamuzi wa
kufuta uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kura kuongezeka katika baadhi ya
majimbo kisiwani Pemba na pia baadhi ya makamishna wa Zec kutanguliza
itikadi za vyama hadi kuvua mashati ili kupigana.
Kadhalika,
alisema katika baadhi ya vituo, masanduku ya kupigia kura yaliporwa na
kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ya
uchaguzi na pia, kuna taarifa ya kufukuzwa kwa baadhi ya mawakala wa
wagombea na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Hata
hivyo, waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wakiwamo Umoja wa Ulaya
(EU), Jumuiya ya Madola Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
waangalizi wa Marekani na Uingereza, katika ripoti zao wamesema uchaguzi
wa Zanzibar mwaka huu ulikuwa huru na wa haki na kutaka Zec ikamilishe
kazi ya kuhesabu kura na kumtangaza mshindi.
No comments:
Post a Comment