Katibu
Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza
(Kulia) akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi
wa vyama vya wasanii yaliyoandaliwa na Baraza hilo mapema wiki hii.
Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utamaduni
anayeshughulikia Lugha kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bi. Shani Kitoga
Msanii
mkongwe wa Sanaa za Maonesho Bw. Kassim Mbelemba maarufu kwa jina la
Mzee Jangala akipokea cheti chake kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Utamaduni anayeshughulikia Lugha kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Shani Kitoga baada ya kumaliza mafunzo
ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya wasanii yaliyoandaliwa na
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii.
Mwezeshaji
wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya Wasanii katika
eneo la Hakimiliki na Hakishiriki Bw. John Kitime akipokea zawadi kutoka
kwa mmoja wa viongozi wa vyama vya wasanii baada ya kutoa mafunzo kwa
viongozi hao.
Viongozi
wa vyama vya Wasanii walioshiriki mafunzo ya Kujengewa Uwezo wakiwa
kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi Bi. Shani Kitoga
IMETOLEWA NA KITENDO CHA HABARI NA MAWASILIANO, BASATA.
BARAZA
la Sanaa la Taifa (BASATA) limewapa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo
katika maeneo mbalimbali viongozi wa vyama na taasisi zinazojihusisha na
wasanii ili kujenga ufanisi zaidi katika sekta ya Sanaa.
Mafunzo
hayo yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumanne hadi Alhamisi ya wiki
hii yalijikita katika kuwajengea uwezo Wasanii kwenye maeneo ya uandaaji
bajeti, uandaaji wa mipango mikakati na sheria ya hakimiliki na
hakishiriki na mikataba kwenye kazi za Sanaa.
Akizungumza
kwenye hafla ya kuyafunga mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa BASATA
Godfrey Mngereza alisema kwamba ana matumaini makubwa kwamba mafunzo
haya kwa viongozi wa wasanii yataamsha ari katika utawala na utendaji wa
sekta ya Sanaa na kufanikisha kupiga hatua kwa sekta hii muhimu.
“Nina
imani katika mafunzo haya tutawaona viongozi wa wasanii mnakuwa na
mipango ya muda mrefu, wa kati na mfupi maana hakuna jinsi tunaweza
kuwaongoza wasanii bila kuwa na mipango” alisisitiza Mngereza.
Kuhusu
suala la hakimiliki, hakishiriki na mikataba kwenye kazi za Sanaa
alisema kuwa ni tatizo linalowakumba wasanii wengi hivyo imani ya
BASATA ni kuona viongozi hawa waliopatiwa mafunzo wanakuwa msaada kwa
wasanii walio chini ya vyama vyao.
“Suala
la hakimiliki linamgusa kila msanii, naamini kwenye suala hili
mmejifunza vya kutosha. Aidha, mmejifunza suala la mikataba katika kazi
za Sanaa, nawaomba muwe mabalozi katika kuwaelimisha wasanii umuhimu wa
mikataba katika kazi wanazozifanya” Aliongeza Mngereza.
Awali
akiongea kabla ya kukabidhi vyeti kwa washiriki, mgeni rasmi ambaye
alimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Shani Kitoga aliwataka viongozi hao
kuzingatia mafunzo waliyoyapata na kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa
mabadiliko kwenye sekta ya Sanaa.
“Sanaa
tunasema ni kazi hivyo lazima mafunzo haya mliyoyapata myatafsiri
katika vitendo kwa kuonesha utendaji kazi ulio bora na unaozingatia
mipango” alisema Bi. Kitoga.
Akiongea
kwa niaba ya viongozi wa wasanii zaidi ya arobaini (40) waliohudhuria
mafunzo hayo, Msanii mkongwe wa Sanaa za Maonesho Kassim Mbelemba
maarufu kwa jina la Mzee Jangala alilipongeza BASATA kwa kuandaa mafunzo
hayo na kuwaeleza wasanii kuwa sasa hakuna sababu ya kulalamika bali
kuyafanyia kazi yale waliyojifunza.
Mafunzo
haya ambayo ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa BASATA
yaliwezeshwa na wakufunzi Rashid Masimbi ambaye ni mtaalam wa kuandaa
mipango mikakati, Mrisho Mtumwa ambaye ni mtaalam wa kuandaa bajeti na
John Kitime ambaye ni Msanii na mtaalam wa masuala ya hakimiliki na
hakishiriki.
No comments:
Post a Comment