KATIKA
hali inayoonyesha ni joto kali la kuwatumikia Watanzania, Mkuu wa Mkoa
wa Kilimanjaro, Amos Makalla, amepiga marufuku likizo za Wakuu wa
wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwenye mkoa wake ili kutekeleza
kwa vitendo hotuba na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dr John Pombe Magufuli.
RC
Makalla aliyasema hayo jana katika kikao cha kazi na wakuu wa wilaya,
wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara wa halmashauri na Kamati ya
Ulinzi na usalama ya mkoa huo kwa ajili ya kupeana mikakati ya majukumu
ya kuwatumikia Wana Kilimanjaro na Watanzania kwa ujumla, ikiwa ni hatua
nzuri ya kwenda na kasi ya Dr Magufuli.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla, akizungumza na Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi na Wakuu wa Idara katika Mkoa huo ili kujipanga katika
majukumu mbalimbali ya kuwatumikia wana Kilimanjaro na Watanzania kwa
ujumla. Picha na Mpiga Picha Wetu.
Baadhi
ya watendaji wa Mkoa Kilimanjaro wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa
huo, Aamos Makalla alipozungumza nao jana. Katika kikao hicho, RC
Makalla alipiga marufuku likizo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na
Wakuu wa Idara ili kujipanga na maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli.
Alisema
kuwa Dr Magufuli ameagiza mambo mengi mazuri na yenye kuhitaji utendaji
uliotukuka, ikiwamo elimu bure, mikakati ya kubana matumizi, kupambana
na maradhi mbalimbali, ugonjwa wa kipindupindu, usimamizi wa pembejeo na
kuzuia pia matukio mbalimbali yenye kugharimu pesa, sanjari na
mapambano ya dawa za kulevya na uwadijibikaji kazini.
“Hakuna
muda wa kupoteza katika kufanyia kazi maagizo ya rais Magufuli, hivyo
sote kwa pamoja tunapaswa kujipanga na kwenda na kasi ya serikali yetu
ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua kubwa kama yalivyokuwa
makusudio yetu ya kuhakikisha watoto wanasoma bure, hivyo sitaki kusikia
likizo kutoka kwa Ma DC, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara katika Mkoa wetu
wa Kilimanjaro. “Suala la kubana matumizi, pembejeo kwa wakulima, vita
ya madawa ya kulevya na mengineyo yanapaswa kuanza sasa, huku
tukihakikisha kwamba maadhimisho ya siku ya Uhuru yanajikita zaidi
kwenye suala zima la usafi kuanzia kaya, mtaa au kijiji na kwingineko,”
Alisema Makalla.
Katika
hatua nyingine, RC Makalla alionyesha kukerwa na ugonjwa wa kipindu
kipindu na kusema kuwa kamwe hataki kuona ugonjwa huo unaingia kwenye
Mkoa wake wa Kilimanjaro, akiwataka wataalamu wa afya na watendaji wa
serikali kujipanga kikamilifu.
Kwa
mujibu wa Makalla, endapo watajipanga imara katika suala zima la usafi,
usimamizi wa rasilimali na utendaji uliotukuka katika maeneo yao, Mkoa
huo utazidi kupiga hatua kubwa kiuchumi, hivyo kufanikisha kwa vitendo
dhamira kubwa ya Dr Magufuli ya kuwakwamua wananchi wake na Watanzania
kwa ujumla. RC Makalla ni miongoni mwa viongozi wa juu wanaopambana
kwenda na kasi ya Rais Magufuli, ikiwa ni siku chache tangu alipoapishwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wananchi wengi
wakionyesha kuwa na Imani kubwa na rais huyo wa awamu ya tano.
No comments:
Post a Comment