CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeliomba Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufuatilia na kumchukulia hatua mtu aliyesambaza ujumbe katika mitandao ya kijamii, kuuchafua uislamu na kiongozi mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na chama hicho jana,
ilieleza kuwa, ujumbe huo kupitia mitandao ya kijamii ikiwamo Whatsapp,
ilieleza Zitto ni mdini na kwamba ni jukumu la waislamu katika jimbo
analowania la Kigoma Mjini, kuhakikisha wanamchagua kwa sababu ya
Uislamu wake.
“Kama chama tumepokea ujumbe huo kwa masikitiko makubwa huku
tukishindwa kuelewa nia halisi ya mwandika ujumbe katika kulinda amani
ya nchi yetu, hasa wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa
madiwani wabunge na rais,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa
Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis.
Aliziomba mamlaka husika, kufuatilia suala hilo kwa kina na kuchukua
hatua za kisheria kwa muhusika kwani ACT-Wazalendo inatambua uadilifu wa
kiongozi wao Zitto katika kusimamia misingi ya haki kwa watanzania wote
hivyo si haki kuchafuliwa kwa misingi ya dini.