151007194612_tanzania_certificates_512x288_bbc_nocredit
Mwanamke akiwa amembeba mtoto wake na cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo katika picha hii ya Mwanamama huyu wa Kitanzania. ( BBC SWAHILI)
Mfumo wa uandikishaji vyeti vya kuzaliwa huko nchini Tanzania kwa kutumia simu za mkononi ulioanzishwa na mamlaka ya uzazi na vifo nchini humo RITA mwaka 2013 umepunguza idadi ya watoto wengi wenye umri wa chini ya mitano ambao hawakuwa na vyeti hivyo.
Hata hivyo, zaidi ya asilimia 80 ya watoto wa vijijini chini ya umri wa miaka mitano nchini Tanzania bado hawana vyeti vya kuzaliwa. Hali hiyo ni matokeo ya wazazi waliowengi kujifungua majumbani na kushindwa kufuatilia jinsi ya kuweza kujiandikisha kutokana na umaskini, umbali wa vituo, na uelewa mdogo wa faida zake.
Kumiliki cheti cha kuzaliwa Tanzania ni jambo muhimu. Mtoto anapata haki za msingi na kufurahia matunda ya nchi yake iwapo atakuwa ametambulika kihalali katika nchi aliyozaliwa.
“Tangu wazazi wangu walipofariki nilipokuwa mdogo sikuweza kupata cheti changu cha kuzaliwa na hakukuwa na mtu muhimu wa kufuatilia cheti changu, hivi sasa nahitaji kusoma, kupiga kura, kadi ya utambulisho wa taifa na misaada mingi ya kunikwamua kimaisha lakini nilikosa huduma hizo mwanzo, hivyo nimekua mkubwa wa kujitegemea nitafanya jitahada nipate haki yangu ya msingi”, anasema binti Innocensia Leizer mwenye umri wa miaka 18..
Vyeti hivi pia vinafaida katika Elimu,ambapo mtoto hawezi kupata elimu ya aina yeyote kuanzia ngazi ya msingi mpaka chuo kikuu kama hatokuwa na cheti cha kuzaliwa. Pia ni muhimu katika kutafutia hati za kusafiria (Passport),hakuna sheria inayoruhusu mtu kupata passport kama hana cheti cha kuzaliwa, hii inasaidia kutambua kama muombaji anatambulika na serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania.
Katika huduma za afya cheti hiki pia ni muhimu kwenye masuala ya afya, baadhi ya huduma za kiafya hazipatikani bila ya cheti cha kuzaliwa. Vitambulisho vya utaifa na vya kupigia kura; vitambulisho hivi ni muhimu kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi, hauwezi kupata kadi yako ya utambulisho wa taifa pasipo na cheti cha kuzaliwa,hivyo hiki ni cheti mhimu sana.
Chanzo: BBC SWAHILI.