UKAWA Watishia Kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Jumapili - LEKULE

Breaking

22 Oct 2015

UKAWA Watishia Kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Jumapili


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachoungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimetishia kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi amesema wanadhamilia kutoshiriki katika uchaguzi huo kutokana Tume yaTaifa ya Uchaguzi (NEC) kutokuwa na msimamo katika kazi zake.

Anasema zikiwa zimebaki siku tatu wananchi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu lakini NEC hadi sasa haina msimamo na kuonekana kuyapuuza madai mengi yenye hoja yanayotolewa na Ukawa.

Akiyataja baadhi ya madai ambayo NEC imeyapuuza ni kutotoa ushirikiano wa kufafanua juu ya upigaji kura kwa watu ambao hawakuona majina yao kwenye daftari la kupiga kura na kutotoa sababu ya utofauti wa namba za kupigia kura kutoka kwenye daftari na kwenye kitambulisho.

Munisi ameongeza kuwa, NEC wamepuuza kutoa ufafanuzi juu ya picha ambazo haziitajiki katika upigaji kura, kutoa ufafanuzi juu ya listi mpya ya wapiga kura iliyosemwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, kwamba kutakuwa na watu wa ziada ambao hawapo kwenye daftari, Je, wanatoka wapi na wapo wangapi? Amehoji.

“Kwa mtindo huu ambao NEC inaenda nao wa kukubali watu wasiokuwa kwenye daftari wapige kura na hata wasiokuwepo kwenye orodha wapige kura mbona hawakutushirikisha sisi wadau wa uchaguzi? Inaweza kupelekea uvunjifu wa amani. Hilo ndio bao la mkono ambalo lilisemwa na hatutaki litokee,” anasema Munisi.

Munisi amesema sababu nyingine kubwa ambayo inaweza kupelekea wasishiriki kwenye uchaguzi ni kuhusu madudu yaliyopo ndani ya daftari la wapiga kura, ambapo hadi sasa NEC haijatoa jibu linaloeleweka juu ya makosa ambayo yalionekana kwenye daftari.

Sababu nyingine ya kutaka kutoshiriki amesema, “Hatuna imani na ujumlishaji wa matokeo ya kura kwa njia ya mashine zao za kujumlisha kwani zinamapungufu mengi. Tuliomba tume itumie njia ya kawaida kwa njia ya kalukuleta ili kila mtu alidhike lakini walidai tunawaingilia kazi zake. Sisi hatutakubali,” amesema Munisi.

Kwa mujibu wa Munisi amesema, hadi sasa bado wanaendelea na uchunguzi kwenye madaftari ya wapiga kura ambapo amesema wameshakagua katika mikoa tisa na kubaini matatizo mengi zaidi yakiwemo ya picha hewa, picha za watu wawili na majina ya kiume kwenye picha za kike.

“Hapo hatujafanya katika majimbo yote tulifanya baadhi. Bado tunaendelea na uchunguzi hadi kesho, tukiona makosa yanazidi kiwango cha kufanya uchaguzi usiende vizuri basi tunaiomba NEC ipeleke uchaguzi mbele,” amesema Munisi.


Aidha, ameitaka NEC kutoa orodha maalumu ya vituo vya kupigia kura kwani hadi sasa Ukawa bado hawajajua idadi kamili ya vituo hivyo wanashindwa kuwaapisha mawakala kwa idadi ya vituo kubadilishwa kila siku.

No comments: