Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 imebisha hodi mjini Moshi baada ya mgombea Udiwani kata ya Soweto, Collins Mayyutta kushitakiwa kwa kosa linaloangukia chini ya sheria hiyo.
Mayyuta
alifikishwa kortini jana akishitakiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwenye
makundi ya WhatsApp dhidi ya mgombea Udiwani wa kata hiyo ya Soweto kwa
tiketi ya CCM, Pamela Shuma.
Ujumbe
huo ambao hata hivyo haukuonyeshwa kwenye hati ya mashitaka, ulidai
Pamella alipewa kiasi kadhaa cha fedha na mgombea mmojawapo wa ubunge
Jimbo la Moshi Mjini ili awape wanawake.
Kwa
mujibu wa ujumbe huo ambao pia ulitumwa kwenye mojawapo ya makundi ya
Whatsapp, Pamela hakugawa fedha hizo kwa makundi ya wanawake kitendo
kichofanya mgombea huyo wa ubunge amweke ndani.
Akisoma
mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,Joachim Tiganga, wakili
wa Serikali Lucy Nkyusa, alidai mshitakiwa alisambaza ujumbe huo wa
uongo Oktoba 9 mwaka huu huko Soweto.
Ildaiwa
kuwa siku hiyo, mshitakiwa alisambaza ujumbe huo wa uongo katika
makundi hayo ya WhatsApp huku akijua fika kuwa ni wa uongo na taarifa
zake zilikuwa zikiupotosha umma.
Hata
hivyo, mshitakiwa alikanusha mashitaka hayo na kupewa dhamana kwa
masharti ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini hati ya
dhamana ya maneno ya Sh1 milioni.
Hakimu
Tiganga aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6 mwaka huu wakati
itakapotajwa, baada ya wakili Nkyusa kuijulisha mahakama kuwa upelelezi
wa shauri hilo la jinai ulikuwa haujakamilika.
Mayyutta
anakuwa mtu wa tatu kushitakiwa chini ya sheria hiyo baada ya
washitakiwa wengine wawili kushitakiwa katika mikoa ya Dodoma na Dar es
Salaam wakituhumiwa kukiuka sheria hiyo.
No comments:
Post a Comment