UKAWA : Daftari la Wapigakura Limejaa VITUKO.....Majengo, Wachina na Namba za Pikipiki Zimeandikishwa Kama Wapiga Kura - LEKULE

Breaking

16 Oct 2015

UKAWA : Daftari la Wapigakura Limejaa VITUKO.....Majengo, Wachina na Namba za Pikipiki Zimeandikishwa Kama Wapiga Kura


WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa ndio kwanza imelikabidhi Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, ili kufanyiwa uhakiki, uchunguzi umeonesha daftari hilo ni chafu na haliaminiki.

Siri hii inafichuka siku tisa tu kabla ya Oktoba 25 ambapo Watanzania wapatao milioni 22 wanatarajiwa kujitokeza vituoni kupiga kura ya kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani.

 
Kwa Zanzibar, kutakuwa pia na uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Waakilishi na Madiwani.
 
Hatua hiyo inakuja siku moja tangu Tume ya Uchaguzi iruhusu vyama vya siasa kuchukua daftari hilo ndani ya shinikizo kubwa la viongozi wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
 
Mbele ya waandishi wa habari jana, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi, walisema kumebainika “madudu na upungufu mwingi kwenye daftari. Kwa hakika haliaminiki.”
 
“Tumeanza kulifanyia ukaguzi daftari la Tume baada ya kulipata  Jumatano, na kwa tuliyoyaona, sasa tumeelewa ni kwanini walikuwa hawataki kulitoa mapema,” alisema Prof. Safari ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu nchini.
 
“… ni wazi Tume hii ambayo si tume huru imejiandaa kuhujumu uchaguzi kwa kuwa katika kituo kimoja tu tulichokagua tumeona majina feki mengi yakiwa yameingizwa,” aliongeza Munisi ambaye alisema ukaguzi ulifanywa katika jimbo la Dodoma mjini.
 
Dosari za msingi zilizobainika katika ukaguzi huo ni
  • Majengo kuandikishwa kama wapiga kura. Katika hali ya kushangaza picha za majengo, ikiwemo migahawa zimeonekana kuwa ni sehemu ya majina ya wapigakura wa jimbo la Dodoma Mjini huku zikibeba majina ya watu na namba ya kitambulisho cha mpiga kura.
  • Baadhi ya vitambulisho kuonekana vikiwa na picha mbili: kumekutwa baadhi ya vitambulisho vinachoandamana na picha ya halisi za watu wengine nyuma.
  • Raia wa kigeni kuandikishwa: Kumekutwa majina ya wasiokuwa raia wa Tanzania wamejumuishwa kwenye daftari, majina mengine yakiwa yasiyoeleweka; picha za raia wanaoonekana kuwa wageni kama Wachina na Wazungu zimeonekana zikiwa sehemu ya wapigakura wa Tanzania; na majina yenyewe yana herufi tupu zisizo na irabu na hivyo kushindwa kusomeka. Kwa mfano limekutwa jina lililoandikwa LHPG SVWTN.
  • Picha za pikipiki kutokeza kama majina ya wapigakura: kumekutwa picha za pikipiki zikiwa ni sehemu ya majina ya wapigakura huku majina na picha hizo yakiwa na namba za vitambulisho vya wapigakura.
  • Majina yalioainishwa kuwa ni ya wanaume yana picha za wanawake: baadhi ya majina yalioneshwa kuwa ni ya kiume na kitambulisho kuonesha kuwa jinsia inayomiliki kitambulisho ni ya kiume lakini picha ni za wanawake.
  • Picha za wapigakura kupigwa katika maeneo tofauti ikiwemo sehemu zenye mabati na mbao badala ya kitambaa kimoja kilichokuwa kikitumiwa kwenye vituo vya Tume: picha za baadhi ya wapigakura zimeonekana kwa mwonekano tofauti wa nyuma (background), ikiwemo kupigwa kwenye sehemu za mabati na mbao hivyo kuzua hofu kuwa huenda uandikishwaji uliendelea katika maeneo mengine baada ya muda wa uandikishaji kumalizika.
Prof. Safari alisema kufuatia uchafu wa daftari, wanaandaa barua kwenda jumuiya za kimataifa ili kuzitahadharisha namna ambavyo serikali ya Chama Cha Mapinduzi inavyoshirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuvuruga uchaguzi.
 
“Leoleo tunaandika barua na kuzituma mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, tunaipelekea pia Jumuiya ya Madola, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa kuwajulisha waone mbinu chafu za CCM kutafuta ushindi wa goli la mkono… wanajiandaa kuiingiza nchi katika machafuko,” alieleza Prof. Safari.
 

Munisi alisema wanaitaka tume ya taifa ya Uchaguzi kutoa majibu juu ya daftari hilo na kulirekebisha haraka sana kabla hawajatangaza uamuzi mwingine watakaouchukua iwapo hawataridhishwa na hatua za NEC.

No comments: