Tundu Lissu ‘anusa’ bao la mkono Singida Mashariki - LEKULE

Breaking

23 Oct 2015

Tundu Lissu ‘anusa’ bao la mkono Singida Mashariki


Mgombea ubunge wa jimbo la Singida mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu  Antiphas Mughwai Lissu, amesema kwamba anahofia uchaguzi mkuu  hautakuwa huru na wa haki akidai kwamba Jeshi la Polisi limeandaliwa kuhakikisha yeye hatangazwi kuwa mshindi.

Lissu alisema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani humo ambapo alibainisha kuwa amepata taarifa kupitia njia ya simu kutoka kwa meneja  wa mkoa wa benki moja mjini hapa na askari polisi wawili, kwamba jeshi la polisi limeandaa nguvu kubwa kupindua maamuzi ya wapiga kura, ili mgombea wa CCM atangazwe mshindi

Tundu  Lissu ambaye ni Mwanasheria mkuu wa CHADEMA, alisema kwa nyakati tofauti, alipigiwa simu na askari polisi wawili akiwemo wa FFU, na kumpa taarifa ile ile aliyopewa na meneja wa benki.

Alisema askari hao walimwambia kuwa jeshi la polisi litatumia magari matatu ya dareya (yanayotumika kumwaga maji ya kuwasha) na kundi kubwa la askari na kwamba wameagizwa na viongozi wao,wahakikishe liwalo na liwe, yeye (Tundu) hatangazwi kushinda ubunge.

Mgombea huyo alisema kwa akili ya kawaida, jeshi la polisi halipaswi kutuma nguvu kubwa jimbo la Singida mashariki ambalo toka kampeni zianze, hapajatokea tukio au dalili za uvunjivu wa amani.

Katika hatua nyingine, Tundu Lissu ameahidi kwamba endapo atashindwa kihalali, atakubaliana na matokeo na hatakuwa na kinyongo chochote.Lakini endapo atashindwa kwa mbinu chafu, hatakubaliana na matokeo hayo machafu.

Naye  Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Sedoyeka, alisema wamemtaka Lissu kwa kuwa ni mwanasheria, athibitishe tuhuma zake hizo, ndipo jeshi la polisi liweze kuchukua hatua stahiki.


Katika jimbo hilo  Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemsimamisha  Bw.Jonathan Njau kupambana na Tundu Lissu katika uchaguzi huu.

No comments: