MBUNGE wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete amesema hana chuki kwa wale ambao hawakumpigia kura kwenye uchaguzi uliofanyika Jumapili kwani hizo ni changamoto za uchaguzi.
Aliyasema
hayo jana kwenye Uwanja wa Miembe Saba mjini Chalinze wakati wa mkutano
wa hadhara wa kuwashukuru Wanachalinze kwa kumchagua kuwa mbunge kwenye
Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili.
Ridhiwani
alisema licha ya baadhi ya maeneo kutompigia kura za kumchagua kuwa
mbunge, lakini atawatumikia wananchi wote bila ya kujali kama walimpigia
kura au la kwani kila mtu ana haki ya kumpigia kura mgombea yeyote
anayempenda.
“Nawashukuru
wananchi wote walionipigia kura na hata wale ambao hawakunipigia kura
kwani hiyo ndiyo demokrasia nitahakikisha nawahudumia wananchi wote bila
ya kuwabagua nitahakikisha napeleka maendeleo kwa watu wote wa jimbo
hili,” alisema Ridhiwani.
Alisema
kutopigiwa kura kwa wingi siyo sababu ya kuwagawa wananchi kwani hizo
ni changamoto za uchaguzi ambao unakuwa na mambo yake ambapo baadhi ya
maeneo walipiga kura kwa kuzingatia ukabila.
“Sitakuwa
na chuki wala hasira kwa wale ambao hawakunipigia kura nitashirikiana
nao katika suala la maendeleo ili kuhakikisha jimbo letu linakuwa na
maendeleo na wananchi wanaboresha maisha yao ili yasonge mbele,” alisema Ridhiwani.
Aidha,
alisema atahakikisha Mji wa Chalinze ambao umekuwa Halmashauri ya Mji
Mdogo unajengwa kwa kuwekewa huduma muhimu ili wananchi waboreshe
biashara zao hasa ikizingatiwa kuwa mji huo ni wa kibiashara.
“Moja
ya mambo nitakayoyafanya ni kufanya Chalinze kuwa makao makuu ya
Halmashauri hiyo na baadaye kuwa wilaya kwani mchakato unaendelea na
tunaamini baada ya muda tutapewa wilaya hivyo tutaweza kujitegemea na
kujiimarisha kiuchumi,” alisema Ridhiwani.
Alibainisha
kuwa wananchi wasiwe na wasiwasi kwani kukichagua Chama Cha Mapanduzi
CCM ni kuchagua maendeleo hivyo wasubiri kuona jinsi serikali mpya
itakavyofanya kazi kwani kwao ni kazi tu.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa CCM Chalinze, Nasa Karama alisema mbunge
huyo ameonesha uwezo mkubwa kwani kwa kipindi alichochaguliwa cha mwaka
mmoja na miezi mitatu amefanya mambo makubwa ambapo alitumia ziadi ya Sh
bilioni moja na zaidi miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment