Rais Jakaya Kikwete, jana amezindua mfumo wa usajili wa kampuni kwa njia ya mtandao utakao ondoa urasimu, rushwa na usumbufu kwa wananchi wanaotaka huduma hiyo. Awali watu walilazimika kusafiri hadi Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Kabla ya kuzinduliwa kwa mfumo huo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi, alisema kazi ya mtandao huo ni kusajili, kulipia na baadaye kupewa cheti cha usajili ndani ya muda mfupi.
Uzinduzi huo ulifanyika wakati wa mkutano wa tisa wa serikali na taasisi binafsi, ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, ukiwa na lengo la kupokea utekelezaji kutoka kwa wizara, taasisi na wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali yaliyojadiliwa katika mkutano wa nane mwezi Septemba, mwaka huu.
"Mfumo huu utaondoa rushwa kwa kuwa mwenyekutaka kusajili kampuni hatakuwa na haja ya kuonana na mtumishi moja kwa moja, ili kusajili ni lazima uingie kwenye tovuti ya Brela,"alisema.
Kanyusi alisema mfumo huo umetengenezwa na vijana wa kitanzania kwa kutumia mapato ya ndani na kuzitaka taasisi nyingine nchini kuiga kwa kutegemea fedha za nje kutekeleza majukumu yao na kwamba kwa rasilimali za ndani, taifa linaweza kupiga hatua na kuendekeza misaada au mikopo ya nje ni kurudi nyuma.
Baada ya kuzindua mfumo huo, Rais Kikwete alisema umerahisisha maisha ya Watanzania ambao walilazimika kusafiri hadi Brela kushughulikia usajili.
Katibu Mkuu wa TNBC, Raymond Mbilinyi, alisema kuna mafanikio makubwa ambayo yatarahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini.
Aliyataja kuwa ni kitengo cha kushughulikia uwekezaji wa wazawa (local content unity), ambacho kimekubaliwa kiwe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Taifa la Uwezeshaji.
Alisema eneo jingine ni urasimu katika kufanya biashara, ambazo ni uwepo wa sheria nyingi zinazokinzana na kwamba moja ya majukumu yaliyoelekezwa kwa wizara ni kuangalia jinsi ya kuainisha sheria ili iwe rahisi kwa mfanyabiashara kujua ni ipi itamsadia kufanya biashara.
"Cha muhimu zaidi pamoja na dunia inavyoenda tunahitaji kuwa na mfumo rahisi wa kumuwezesha mfanyabiashara popote duniani kupata taarifa za biashara inavyofanyika na kupata leseni kwa urahisi, tunakwenda kidijitali badala ya kuwa na utaratibu wa kuandika karatasi, Wizara ya Viwanda na Biashara inatengeneza mfumo wa kurahisisha wafanyabiashara ndani na nje kupata taarifa na leseni kwa urahisi zaidi,"alisema.
Alisema kuweka mfumo mmoja wa taasisi zinazomuhudumia mfanyabiashara kutoa huduma katika eneo moja na badala ya kumpa usumbufu wa kwenda katika kila taasisi.
"Kuna Osha,TRA, Brela na taasisi nyingine nyingi, hizo zote zinaweka mazingira magumu, tuje na mfumo ambao wafanyabiashara wanaweza kujipima katika maeneo yanayohitajika,” alisema.
Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya TNBC, Balozi Ombeni Sefue, alisema mkutano huo pia umeangalia namna ya kukuza utalii nchini kwa kuboresha mazingira, ikiwamo kuangalia utathimini wa msimu kwa kupunguza kodi kipindi ambacho siyo msimu wa utalii na kuiweka katika Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alisema mazingira ya biashara yanarahisishwa kwa kuhakikisha serikali inaweka mfumo mmoja wa kumhudumia mfanyabiashara kuliko kuwa na taasisi nyingi na kumlazimu mfanyabiashara kuzitembelea zote.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja, alisema mazingira ya kufanya biashara Tanzania ni magumu kutokana na jinsi ya kupata leseni, namba ya usajili na usajili wa kampuni na jina la biashara.
Alisema serikali inatakiwa kupunguza au kuweka katika mfumo mmoja taasisi zinazomuhudumia mfanyabiashara kwa kuwa zote zipo chini ya serikali.
Mkutano huo umewakutanisha mawaziri, makatibu wakuu, Shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).