Shamma Gwajima (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kushoto ni Raphah Gwajima. |
Wakizungumza mapema leo hii na waandishi wa habari Idara ya Habari Maelezo, Jijini Dar, watoto hao waliojitambulisha kwa majina ya Shamma Gwajima (18) na Raphah Gwajima (17) walisema kuwa baba yao ambaye ni kaka wa Askofu Gwajima alifariki dunia mwaka 2008 mkoani Mwanza kwa maradhi ambapo Askofu Gwajima wanayemwita baba mdogo alifika msibani hapo na kuwataka ndugu na marafiki waliokuwa wakiomboleza kifo cha mpendwa wao wasihuzunike kwa kuwa marehemu hakuwa amekufa bali amelala tu.
“Mchungaji Gwajima alitukataza tusilie na tusihofu kwa chochote kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kumuombea marehemu hadi afufuke. Kauli hiyo ilitufanya tuanze kufurahi na akaushika mwili wa marehemu katikati ya umati wa watu na kuanza kuutikisa akimtaka baba yetu aamke lakini hakuamka,” alisema Shamma.
Watoto hao walidai kuwa tangu siku hiyo Gwajima aliondoka kimyakimya na kuingia mitini na kudai kuwa jambo hilo limewaathiri kihisia na kisaikolojia na wanajiandaa kumshtaki kutokana na usumbufu aliowasababishia katika kipindi kigumu cha msiba wa baba yao.
Watoto hao walienda mbali zaidi na kudai kuwa waliamua kukaa kimya wakiamini Askofu Gwajima ambaye ni baba yao mdogo anastahili heshima ya kichungaji mbele za watu, lakini walidai kuwa wanashangazwa na mambo ayafanyayo hivi karibuni kama vile kuwatukana watumishi wenzake na kutoa siri za waumini wanaoenda kwake kwa ajili ya kupata huduma za maombezi.
Aidha walidai kuwa Askofu Gwajima ni tapeli kwa kuwa anatumia huduma ya kufufua misukule ‘hewa’ kwa maslahi yake binafsi na kuitaka serikali iingilie kati kumchukulia hatua huku wakiitaka jamii isikubali udanganyifu wa askofu huyo kwa kuwa kama kweli anafufua watu basi angemfufua kaka yake.
“Je, misukule ambayo anatangaza ameifufua, tujiulize kabla ya kufariki ilikuwa ikiishi wapi? Na, je, kuna vyeti vya kifo vinavyothibitisha kama watu hao wanaofufuliwa walikufa kweli? Je, ndugu wa hiyo misukule wapo?” walisema watoto hao na kuongeza kuwa kutokana na kushindwa kwake kumfufua baba yao, Gwajima amewatelekeza kwa kutowapa msaada wowote licha ya yeye kuishi maisha ya kifahari.