Mbunge ashambuliwa kwa kuandaa nyama ya ng’ombe - LEKULE

Breaking

11 Oct 2015

Mbunge ashambuliwa kwa kuandaa nyama ya ng’ombe

Ng'ombe
Ng'ombe huchukuliwa kuwa mnyama mtakatifu katika dini ya Kihindi
Wabunge wa chama tawala nchini India cha Bharatiya Janata Party (BJP) wamempiga mbunge Mwislamu kwa kuandaa nyama ya ng’ombe katika sherehe.
Abdul Rashid Ahmed, mbunge wa jimbo la Kashmir, alipigwa mangumi na mateke kabla ya kuokolewa na wabunge wa upinzani.
Kanda ya video ilionyesha wabunge kadha wa BJP wakimpiga Abdul Rashid, katika bunge la majimbo ya Jammu na Kashmir kwa kuandaa, sherehe ya “ulaji nyama ya ng’ombe”.
Rashid alikuwa ameandalia watu nyama hiyo kulalamikia kushambuliwa na kuuawa kwa mwanamume mmoja wiki iliyopita baada ya uvumi kuenea kwamba alikuwa akila nyama ya ng’ombe.
Ahmed aliambia AFP alishambuliwa na wabunge kati ya 10 na 14 wa BJP punde tu alipoingia bungeni na kuongeza kuwa hata alihofia maisha yake.
Chama cha BJP kinachotawala nchini India huwa na Wahindi wengi.
Ng’ombe ni mnyama mtakatifu kwa mujibu wa dini ya Kihindi na huwa haramu kula nyama yake.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuona jambo kama hili katika bunge lolote lile. Sasa nitampiga kila mtu anywaye pombe au kula nyama ya nguruwe?” alishangaa kiongozi wa upinzani
Omar Abdullah, ambaye ni Mwislamu nje ya majengo ya bunge hilo mjini Srinagar. Huwa ni haramu kula nyama ya nguruwe kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.
Wabunge wa chama chake waliondoka bungeni kulalamikia kisa hicho.
Majimbo mengi nchini India yana sheria kali zinazozuia uuzaji na ulaji wa nyama ya ng’ombe.
Majuzi, visa vya watu kushambuliwa kwa kula nyama ya ng’ombe vimekuwa vikiongezeka.
Mwezi uliopita, mwanamume mmoja Mohammad Akhlaq, 50, alipigwa na kuuawa baada ya uvumi kuenea kwamba alikuwa amekula nyama ya ng’ombe.
Mwanawe wa kiume wa miaka 22 alijeruhiwa vibaya.
Watu wanane wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo yaliyotekelezwa Septemba 28.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ameshutumu mauaji ya mwanamume huyo Mwislamu, akisema Waislamu na Wahindi nchini humo wanafaa kushirikiana kuangamiza umaskini badala ya kupigana wenyewe.

Ng'ombe
Chama cha BJP kinataka ulaji nyama upigwe marufuku kote nchini humo.
Bw Modi amekabiliwa na shinikizo za kumtaka ashutumu maaji hayo.
Tangu aingie mamlakani mwaka jana, chama chake cha BJP kimekaza sheria dhidi ya ulaji wa nyama ya ng’ombe. Chama hicho kinataka ulaji nyama upigwe marufuku kote nchini humo.

No comments: