Magufuli: Mafisadi Wamewafanya Wananchi Waichukie Serikali Yao.....Niombeeni ili Nikiingia Ikulu nisiwe na Kiburi - LEKULE

Breaking

6 Oct 2015

Magufuli: Mafisadi Wamewafanya Wananchi Waichukie Serikali Yao.....Niombeeni ili Nikiingia Ikulu nisiwe na Kiburi


Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amefichua kuwa vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi na vigogo wa serikali ndiyo sababu ya kuchukiwa kwa serikali ya chama tawala.
 
Kutokana na hali hiyo,  amewaomba wananchi wampigie kura nyingi za ndiyo ifikapo siku ya uchaguzi, Oktoba 25, mwaka huu ili awachukulie hatua na kukomesha hali hiyo.

Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni mjini Hanang, mkoa wa Manyara jana, Dk. Magufuli alifafanua kuwa yeye ni tingatinga na Watanzania wakimpigia kura nyingi na kumuingiza Ikulu atawaonyesha namna atakavyosafisha mafisadi serikalini na mwishowe kuwezesha maisha bora kwa kila mmoja.

Dk. Magufuli alisisitiza kuwa akiingia Ikulu, kamwe hatakuwa na msamaha dhidi ya mafisadi na wala rushwa kwani mara zote wamekuwa chanzo cha kukwamisha huduma za jamii zinazotolewa na serikali na kusababisha wananchi waichukie serikali yao.

Alirudia kauli yake anayoitoa karibu katika kila mkutano kuwa ataanzisha mahakama ya mafisadi ili kuhakikisha analinda rasilimali za umma ambazo zimekuwa zikiibwa na watu wachache.

Alisema anatambua kuwa hivi sasa Watanzania wamechoshwa na maisha duni, hivyo wanahitaji kuwa na rais kama yeye ambaye atasimamia mabadiliko ya kweli ili kila Mtanzania afaidi maisha bora .

“Niombeeni ili nikiingia Ikulu nisiwe na kiburi... nataka niwatumikie Watanzania wote bila kujali vyama vyenu, maana mmeteseka sana na shida zilizosababishwa na mafisadi. Vitu vimepanda bei kwa sababu ya ufisadi.  Nataka kukomesha yote hayo,” alisema.

Aliongeza kuwa anatambua mikakati ya mafisadi ambao wamejipanga kutoa rushwa ili kuwarubuni wananchi wawachague kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

“Fedha chukueni, lakini kura ni kwa Dk. Magufuli tu. Zile fedha watakazogawa ni zenu. Walizichukua kwa wizi walipokuwa madarakani, zichukueni, lakini tarehe 25 wataisoma namba,” alisema.