MAGUFULI: Mabadiliko Ya Kweli Hayawezi Kuletwa Kwa Kuzungusha Mikono - LEKULE

Breaking

20 Oct 2015

MAGUFULI: Mabadiliko Ya Kweli Hayawezi Kuletwa Kwa Kuzungusha Mikono



MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa kwa kuzungusha mikono, bali yatakuja kwa kufanya kazi.

Kutokana na hali hiyo, amesema yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko ya kweli yanayokwenda na vitendo katika kujenga uchumi wa nchi na watu wake.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti, alipokuwa akizungumza wakati wa  mikutano ya kampeni iliyofanyika katika majimbo ya Buchosa, Geita na Busanda.

Katika mazungumzo yake, Mgufuli aliwataka Watanzania wasidanganywe na baadhi ya wanasiasa wanaowataka wasiipigie kura CCM.

Alisema kwamba, pamoja na baadhi ya wanasiasa kukesha wakihamasisha mabadiliko kwa kutoichagua CCM, jambo hilo halitawezekana kwa kuwa ni sawa na ndoto za mchana.

“Ninasema hapa, eti kuna watu wanahangaika kuzungusha mikono na kusema wanaleta mabadiliko, ni lazima wajue mabadiliko hayawezi kuja kwa mtindo huo.

“China hivi sasa inatisha kwa kuwa na uchumi wa daraja la kwanza duniani na kuna hatari hata ya kutaka kuizidi Marekani.

“Kwa mfumo wao huo, hawakukiondoa madarakani chama tawala ila walifanya mabadiliko ya ndani ya chama na Serikali.

“Ndiyo maana Magufuli ninakuja na mabadiliko ya kwenda ndani ya Serikali na ndani ya CCM. Katika hili, sina mchezo ndugu zangu Watanzania, naomba mniamini,” alisema Dk. Magufuli.

Kwa kuwa Watanzania wameshaamua kumpa urais Oktoba 25, mwaka huu, jambo atakalo anza nalo ni kuunda mahakama ya mafisadi.

Alisema, amezaliwa katika familia maskini na hatakuwa tayari kuona wajasiriamali wadogo wakinyanyaswa na hata kutozwa ushuru ambao umekuwa ukiwakandamiza katika biashara zao.

Alisema anajua eneo la Nkome ni maarufu kwa kilimo cha mananasi daraja la kwanza, lakini bado wakulima wamekuwa wakikosa soko la uhakika.

Kutokana na hali hiyo, atatimiza mkakati wa Serikali yake kwa kujenga kiwanda cha juisi katika  eneo hilo.

“Ni aibu kwa nchi yetu inayozalisha matunda kwa wingi, kukosa kiwanda cha kusindika matunda.

“Napenda kuahidi hapa, nitajenga kiwanda cha juisi kitakachosaidia wakulima wa mananasi kuwa na soko la uhakika badala ya kwenda Geita mjini au Mwanza.

“Tukijenga kiwanda hapa, tutatoa ajira kwa vijana na tutatengeneza juisi yetu badala ya kila siku kuagiza kutoka nje ya nchi, hii ni aibu,” alisema.

No comments: