Magufuli Asimamisha Jiji La Dar.......Asema Tanzania Inahitaji Rais Mkali. CHADEMA Wampokea Kwa Ishara Ya Vidole Viwili Juu - LEKULE

Breaking

22 Oct 2015

Magufuli Asimamisha Jiji La Dar.......Asema Tanzania Inahitaji Rais Mkali. CHADEMA Wampokea Kwa Ishara Ya Vidole Viwili Juu


Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema nchi inahitaji rais mkali ili mambo yaende huku akishangazwa na mmoja wa vigogo kufungua kesi kupinga mradi wa maji.

Amesema watu wa aina hiyo watakiona na anamuomba Mungu kwa siki tatu zilizobaki apewe urais kwa vile hao ndiyo ataanza kushughulika nao.

Kauli hiyo aliitoa   Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni iliyofanyika   Kigamboni, Mbagala, Temeke, Ubungo na Kinondoni.

Alisema hayuko tayari kuona watu wanaendelea  kupoteza maisha kwa   kipindupindi huku kigogo huyo akikimbilia mahakamani.

Kitendo cha kigogo huyo  kufunga njia ya maji kwa kujenga bomba la majitaka kimesababisha wananchi wa   Dar es Salaam  kupoteza maisha kwa kuugua kipindupindu, alisema.

“Ninajua hapa Temeke kuna mtu amekimbilia mahakamani na kukwamisha mradi wa maji lakini mahakama haitoi haki kwa wakati.

“Zimebaki siku nne ninichague kuwa rais, mtu anachelewesha mradi wa maji kwa kwenda mahakamani ngoja nipate urais. Amejenga juu ya njia ya maji watu wanakufa kwa kipindupindu haki ya Mungu ngoja nipate urais.

“…tunahitaji rais mkali mambo yaende kesi ni lazima iamuriwe kama Serikali tumeshindwa tukate rufaa. Tena huyo mtu aliyefungua kesi ana udugu na mmoja wa wagombea wa Ukawa,” alisema Dk. Magufuli.

Mgombea huyo wa urais alisema  atakapochaguliwa Jumapili atakwenda kuanza na hilo.

“Haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani mradi wa maji una manufaa wao wanakunywa maji ya Kilimanjaro wananchi wanateseka. Lakini watu wachache kwa tamaa zao na madaraka yao wanakwamisha.

“Wanasema mimi ni mkali, hapana nina hofu ya Mungu, tunaomba kesi hii iamuriwe kama tumeshindwa tukate rufaa,” alisema Dk. Magufuli

Mgombea huyo wa urais alisema yeye ni mtu wa uamuzi makini anayekuja kuijenga Tanzania mpya na yenye matumaini kwa watanzania wote.

Alisema anashangazwa na watu wanaohangaika na uamuzi mgumu kwani wanaofanya hivyo ni majambazi, wezi na mafisadi pekee.

Dk. Magufuli, alisema ataongoza taifa kwa umakini kwa kuleta maendeleo ya kweli.

Alisema anashangazwa na watu wanaopita na kujinasibu kwa kuleta uamuzi mgumu wakati ndiyo walioleta matatizo katika nchi na hata kusababisha kero ya umeme kila kukicha.

“Watakuja wapinzani wetu na kusema eti wanakuja na uamuzi mgumu, jamani uamuzi mgumu hufanywa na majambazi, wezi na wauaji wa watu wenye albino. Inashangaza sana hawa watu msiwakubalie hata kidogo.

“… hivi jana itokee upate mume au mke anayetamba kwa kuwa na uamuzi mgumu si atakunyonga kitandani. Eti atafanya uamuzi mgumu mbona hujinyongi kwa kamba?  Mimi kwangu Magufuli kazi tu,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumzia ujenzi wa daraja la Kigamboni, Dk. Magufuli alisema litakamilika mwezi ujao na wananchi wa eneo hilo watavuka bure ila watu wenye magari ndiyo watakaolipa ada.

Alisema yeye ni mtu anayesimamia sheria hivyo katu hawezi kuzivunja   kwa kutoa ahadi za uongo kwa lengo la kutafuta kura za watanzania.

“Daraja la Kigamboni litakamilika mapema mwezi ujao na litakapokamilika wakazi wa Kigamboni watapita bure ila wenye magari watalipia kama ilivyokuwa kwenye kivuko cha pantoni.

“Kigamboni ya sasa imekuwa na maendeleo na kwa sababu mbunge wenu, Dk. Ndugulile (Faustine) ni mfuatiliaji nami nawaomba mumchague ninamuhitaji.

“Alipambana kwa ajili ya yenu na sasa ninasema hapa Rais Jakaya Kikwete amenisaidia sana kwa kuiteua Kigamboni kuwa wilaya nami kazi yangu itakuwa ni kuleta maendeleo ya kweli,” alisema.

Mgombea huyo wa urais alisema kwa mujibu wa sheria, ardhi ni mali hivyo kwa Kigamboni kujengwa mji mpya ni hatua kubwa ya maendeleo.

Dk. Magufuli aliwataka wakazi hao kuhakikisha wanasimamia haki zao ikiwamo kumiliki ardhi yao na hata kushirikiana na wawekezaji.

“Ardhi ni mali na hapa Kigamboni sasa mji mpya   wakija wawekezaji kwanza wawape noti na hata mshirikiane pamoja kutokana na ardhi yenu,” alisema.

Chadema wampokea Ubungo  huku  wakimshangilia  Lowassa
Mgombea huyo wa urais wa CCM alipofika katika Kituo cha Mabasi Ubungo, alisimamishwa na wafuasi wa Ukawa  ambao  walimnyoonshea  vidole  viwili  juu  huku  wakimshangilia  Mgombea  wao  kwa  kuimba  Lowassa!!!  Lowassa!!

Baada  ya  hali  hiyo,Magufuli  aliwasalimia wafuasi  hao  wa  Ukawa  kwa  ishara  ya  salamu  zao  na  kuwaambia  kuwa  maendeleo  hayana chama.

“Maendeleo hayana chama iwe Chadema, CCM, CUF na hata Ukawa mimi kwangu ni kazi tu,” alisema.....Tazama  Video  Hii





No comments: