Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amewataka wananchi kujipanga kufanya kazi kwa sababu Serikali yake haitavumilia watu wavivu.
Akihutubia
mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Misungwi jana, Dk
Magufuli alisema hata vitabu vya dini vimeelekeza kwamba asiyefanya kazi
na asile, hivyo wanaoahidi vitu vya bure wanawadanganya Watanzania.
“Tujipange
kufanya kazi, hata maandiko ya vitabu vitakatifu yanasema, asiyefanya
kazi asile… Misungwi nitaibeba kwa nguvu zangu zote nikichaguliwa,” alisema.
Pia
alisema nyumba za tembe ambazo zinaahidiwa na wagombea wenzake kwamba
zitaondolewa ndani ya siku 100 ni uongo hivyo wasisikilizwe, bali
atakachofanya ni kuhakikisha bei ya vifaa vya ujenzi inapungua na
ameanza na saruji.
Alisema
anatambua kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo la maji na kuwaahidi
wananchi kulishughulikia na wasimsumbue mbunge wao na kwamba anapoahidi
kutoa Sh50 milioni kila kijiji nchini watu wanamshangaa lakini Serikali
ina fedha, nyingine zilikuwa zinatafunwa na mafisadi.
“...Ndiyo
maana baada ya kusikia nimetangazwa mengine yakakimbia… hivi sasa
wanasema Serikali haijafanya chochote wakati wengine wamezeekea humu
mpaka wakang’oka meno na kuwekewa ya bandia, mbona hawakuondoka muda
wote?” alihoji Dk Magufuli.
Mgombea
huyo huku akichomeka lugha ya Kisukuma kila mara, alisema ujenzi wa
barabara ya Usagara – Kisema ukikamilika, malori yatakuwa hayaruhusiwi
kuingia katikati ya mjini wa Mwanza. Aliahidi kufufua viwanda vya
kuchambua pamba ili kuleta mabadiliko ya kweli.
Dk
Magufuli aliahidi kufufua kilimo cha pamba kwa kuhakikisha mkulima
anapata pembejeo na kunufaika na zao hilo na kwamba, haiwezekani pamba
ilimwe Tanzania Ulaya wavae nguo mpya halafu Watanzania waletewe
mitumba.
Hata
hivyo, mgombea huyo akiendelea kutoa ahadi sauti za wanawake zilisikika
zikimtaka kuzungumzia samaki kazi ambayo ndiyo wanayoitegemea kiuchumi,
hivyo akalazimika kutamka kuwa atafuta ushuru unaoonekana kuwa kero.
“Nitafufua Chuo cha Kilimo Ukiriguru na kutumia wataalamu wake kuboresha kilimo cha pamba,” alisema.
Mgombea
ubunge Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga alisema kuna sifa ya Dk
Magufuli ambayo haijatajwa nayo ni ubunifu, kwani alianzisha mfuko wa
kujenga barabara kwa fedha za ndani hali iliyowashangaza wafadhili.
“Hizi
barabara tunazotaja kama siyo yeye zisingekuwapo, mnakumbuka wafadhili
walikuwa wanakataa kutukopesha, akaanzisha mfuko wa kujenga barabara
mpaka wafadhili wanauliza fedha zitakapopatikana, akawaambia tunazo,” alisema.
Kitwanga alimwomba mgombea huyo kuwajengea hospitali ya wilaya na kiwanda cha kusindika nyanya, zao linalolimwa kwa wingi.
No comments:
Post a Comment