Magufuli Apiga Mashambulizi Jimboni Kwa Mbowe......Asema Mbowe ni Mbunge mtalii Anayeshinda Akizurura Ulaya - LEKULE

Breaking

8 Oct 2015

Magufuli Apiga Mashambulizi Jimboni Kwa Mbowe......Asema Mbowe ni Mbunge mtalii Anayeshinda Akizurura Ulaya



Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, ametikisa katika Jimbo la Hai na kumshambulia Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema aliyemaliza muda wake,  Freeman Mbowe  kwamba ni Mbunge mtalii anayeshinda akizurura Ulaya, huku akishindwa kutatua kero za wapiga kura wake.

Akihutubia jimboni humo katika siku yake ya kwanza ya kampeni mkoani Kilimanjaro jana, Dk. Magufuli aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kwamba, walifanya biashara ya hasara kumchagua Mbowe kuwa Mbunge wao kwani hajali maslahi ya wananchi wake.

Awali mgombea huyo wa CCM alipokelewa na umati wa jimbo hilo kwa mabango yenye ujumbe mbalimbali yanayoelezea kero za maji, barabara, elimu na afya, ambayo aliagiza yachukuliwe na msafara wake ili atakapoingia Ikulu azifanyie kazi kero hizo.

Dk. Magufuli alisema wananchi wa Jimbo la Hai wameteseka kwa muda mrefu kwa kuwa na Mbunge ambaye kazi yake imekuwa kuzunguka jijini Dar es Salaam na mataifa ya Ulaya na Marekani, huku jimbo likikabiliwa na matatizo ya kijamii kama maji, elimu na ukosefu wa huduma za afya.

“Ingawa nampenda Mbowe, lakini wananchi wa jimbo hili wanapaswa kufanya mabadiliko kwa kumtosa Mbunge huyo  abaki na nafasi yake ya uenyekiti wa Chadema ili akaimarishe chama hicho na wamchague mbunge wa CCM ambaye atawasaidia,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, Mbowe hawezi kushughulikia masuala ya maendeleo kwa kuwa anakabiliwa na majukumu mengi ya biashara na uenyekiti wa Taifa wa Chadema.

“Mbowe ana nipenda na huwa ana nisifia hadharani kwamba mimi ni mchapakazi na mimi pia nampenda sana lakini kwenye masuala ya maendeleo ya Watanzania sitaweka urafiki achaneni naye na mumchague Dunstan Mallya wa CCM awafanyie kazi watu wa Hai.”alisema mgombea huyo wa CCM.

Alisema hata Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambayo inaongozwa na Chadema imeshindwa kuondoa kero za wananchi na kuongeza kuwa ingawa wilaya hiyo ni ya zamani imebaki nyuma kwa miaka mingi kulinganisha na wilaya mpya.

Akiwahutubia wananchi wa Siha, mkoani hapa jana, Dk. Magufuli alisema ameshajihakikishia ushindi wa kishindo na kudai wapinzani wanamsindikiza na kuwataka wananchi wa jimbo hilo wamchague Agrey Mwanri kwa mara nyingine awe Mbunge wao kutokana na kazi nzuri aliyowafanyia.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Dk. Emmanuel Nchimbi, aliibukia kwenye kampeni za Dk. Magufuli wilayani Siha na baadaye Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro jana na kumrushia makombora mgombea urais  wa Ukawa, Edward Lowassa.

Dk. Nchimbi ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Lowassa kwenye harakati za kuwania kuteuliwa na CCM kuwania urais, alidai Lowassa ni dhaifu na hawezi kuiongoza Tanzania.

Nchimbi alisema Watanzania wanahitaji  Rais aina ya Magufuli ambaye atawaendesha mchakamchaka wa maendeleo na si wagombea wengine ambao historia zao zinaonyesha walishindwa kwenye nafasi za juu walizowahi kushika.

No comments: