Magufuli Afichua Ushauri Aliopewa na Marehemu Dr. Kigoda Kabla ya Mauti Kumkuta - LEKULE

Breaking

15 Oct 2015

Magufuli Afichua Ushauri Aliopewa na Marehemu Dr. Kigoda Kabla ya Mauti Kumkuta


Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli, jana aliwaongoza wanachama wa chama hicho kuupokea mwili wa Dtk. Abdallah Kigoda aliyepoteza maisha nchini India, ambapo alieleza kuwa alimpa ushauri katika kipindi kifupi kabla Mungu hajamchukua.
 
Akiongea na waandishi wa habari, Magufuli alieleza kuwa Marehemu Kigoda alimshauri masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwasaidia wawekezaji na wafanyabiashara wazalendo.
 
Alisema kifo cha Dkt.Kigoda ni pigo kubwa kwa Watanzania wote kwani alikuwa na moyo wa kuwatumikia Watanzania ili wapate maendeleo.
 
"Nitamkumbuka Dkt.Kigoda kwa mengi; ila nakumbuka alipokuwa Apollo nchini India aliposikia naenda jimboni kwake aliomba ruhusa ya siku moja; akaja tukaungana kule jimboni kwake ambapo nilimkabidhi ilani ya uchaguzi kisha akarudi Apollo kuendelea na matibabu", alisema Dkt.Magufuli na kuongeza:
 
"Kabla ya kupelekwa ICU (Chumba cha uangalizi maalumu) alinipigia simu na kunipa ushauri jinsi ya kuwajali na kuwasaidia wafanyabiashara wa ndani; hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwetu".
 
Ombeni Sefue
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kifo cha Dkt.Kigoda ni pigo kubwa kwa Serikali kwani ni Waziri ambaye amefanya kazi kubwa ya kuwatumikia Watanzania.
 
"Kifo chake ni pigo kubwa sana kwa Watanzania na Serikali kwa ujumla kwani ni waziri ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu katika kuwatumikia Watanzania," alisema Balozi Sefue.
 
Mwili wa Dkt. Kigoda uliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam majira ya saa 9 na dakika 35 alasiri kwa Ndege ya Shirika la Emirates.
Mwili huo ulipokewa na viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya siasa.
 
Baadhi ya viongozi walioshiriki kwenye mapokezi hayo ni mgombea urais kupitia CCM, Dkt.John Magufuli,Spika wa Bunge, Anne Makinda pamoja na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe.

No comments: