Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecki Sadiki Akifungua mafunzo ya
siku mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi
wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo jijini Dar es salaam.
Waratibu wa
Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na
Maafisa uchaguzi waliohudhuria mafunzo leo jijini Dar es
salaam kujiandaa usimamizi wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
Oktoba 25 mwaka huu.
Picha/ Aron Msigwa- MAELEZO.
Na.Aron Msigwa- MAELEZO.
Mkuu wa mkoa wa Dar es slaam Said Mecki Sadiki amewataka Waratibu wa
Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya Siasa katika
mkoa huo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa ushirikiano ili
kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa amani na utulivu na kuepusha
manung'uniko yanayoweza kujitokeza.
Akifungua mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa
Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo
jijini Dar es salaam Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Dar es salaam ni
miongoni mwa maeneo yenye wapiga kura wengi hivyo mkoa kwa kushirikiana
na Tume ya uchaguzi umejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wote
waliojiandikisha wanapiga kura kwa amani na utulivu Siku ya uchaguzi
Oktoba 25 mwaka huu.
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri wa mkoa huo ambao ndiyo wasimamizi wa
uchaguzi katika wilaya wanalo jukumu la kuwaita na kuwaelimisha
viongozi wa vyama vya siasa juu ya taratibu na kanuni za kufuata wakati
wa uchaguzi mkuu ili wajenge mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa
ushirikiano.
Aidha, amewasisitiza wasimamizi hao kutojihusisha kwa namna yoyote ile
na kampeni za siasa wakati wa kutekeleza majukumu yao kwani kufanya
hivyo watakuwa wanahujumu ufanisi wa uchaguzi mkuu katika mkoa wa Dar es
salaam.
Ili kudumisha amani na utulivu vituoni amewataka kufanya kazi zao kwa
umakini mkubwa kwa kuwa suala la amani vituoni litakuwa mikononi mwao
wakati wa kipindi chote cha upigaji wa kura Oktoba 25 mwaka huu.
"Simamieni kanuni, sheria na taratibu, msionyeshe upendeleo wowote wala
kufanya kampeni za aina yoyote ile ndani ya vituo vya kupigia kura,
jambo hilo halikubaliki hata kidogo,mfanyeni kazi mliyotumwa ili msiwe
sehemu ya tatizo katika nchi hii" Amesisitiza Sadiki.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza kadi zao za kupigia kura ili
waweze kuzitumia siku ya uchaguzi na kuvionya vikundi, watu au vyama
vinavyojaribu kuwarubuni wananchi kwa kununua kadi zao za kupigia kura
kuacha tabia hiyo.
" Watu wanaofanya hivi wanafanya unyang'anyi, nawataka waache tabia hii
kwani haina tija kwa mamaendeleo ya taifa letu,ukichukua au kuiba kadi
ya mtu unamnyima haki ya kupiga kura muhusika na huo sio uungwana"
Amesisitiza.
Ametoa wito wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kudumisha amani wakati wa
upigaji wa kura na kuwataka wananchi wote waliopanga kufanya vurugu
wakati wa uchaguzi kuacha
"Sisi kama Serikali hatuvumilia aina yoyote ya uvunjifu wa amani,
tutaimarisha ulinzi yapo maeneo korofi ambayo yamekuwa na vitendo vya
uvunjifu wa amani tunayajua, tunawahakikishia wananchi watapiga kura kwa
amani na kurudi makwao wakiwa salama"
Kuhusu waangalizi wa Kimataifa waliowasili nchini ambao baadhi yao
watafanya kazi jijini Dar es salam amesema watafanya kazi zao kwa mujibu
wa taratibu na kanuni walizopewa na Tume na kuongeza kuwa kazi yao
itakua ni kuangalia kama tumnazingatia na kufuata sheria tulizojiwekea
na si kuingilia shughuli za wasimamizi wa zoezi la upigaji wa kura.
"Suala la kusimamia zoezi la upigaji wa kura ni letu wenyewe,
msiwaruhusu waanze kuwapa taratibu za upigaji wa kura wa nchi walizotoka
wala kutoa maamuzi yoyote, kazi yao itakua ni kuangalia mwenendo wa
uchaguzi wetu na si vinginevyo" amesisitiza.
Aidha, amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawapeleka mawakala
wao mapema katika vituo vya kupigia kura kabla ya kuanza kwa zoezi la
upigaji wa kura ili kuondoa manung'uniko yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake Bi. Clesensia Mayala ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu,
Kanda ya Kusini Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema lengo la mafunzo hayo
ni kuwakumbusha wasimamizi na Maafisa uchaguzi kuzingatia na kufuata
taratibu zilizotolewa na Tume ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Amesema katika mafunzo hayo washiriki hao watajadili masuala mbalimbali
ikiwemo wajibu na majukumu ya waratibu na wasimamizi wa
uchaguzi,majukumu ya makarani waongozaji wa vituo vya kupigia kura
,kuangalia fomu zitakazotumika wakati wa upigaji kura,taratibu za
upigaji kura, Fomu zitakazotumika wakati wa kuhesabukura, kujumlisha na
kutangaza matokeo ya Urais,Wabunge na Madiwani.
Amefafanua kuwa wasimamizi wote wa uchaguzi watakua na jukumu la
kuhakikisha kuwa vituo vyote ya uchaguzi vinafunguliwa kwa wakati na
kufungwa kwa kuzingatia muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa wananchi
wote wanatimiza wajibu wao wa kikatiba.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Temeke Bw. Photidas
Kagimbo amesema uchaguzi mkuu katika eneo analolisimamia utafanyika kwa
uhuru na usalama na kuongeza kuwa wamejipanga vyema kuwahudumia wananchi
wote waliojiandikisha ambao watajitokeza kupiga kura siku hiyo.
Amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kupeleka vifaa mbalimbali
katika maeneo mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kupiga kura Oktoba 25
na kufafanua kuwa kazi inayoendelea sasa ni utoaji wa elimu ya mpiga
kura kwa wananchi.
Kuhusu uhakiki wa taarifa za wananchi katika daftari la kudumu la Wapiga
kura kwa wananchi walioshindwa kuhakiki kutokana na sababu mbalimbali
amesema liko mikononi mwa Tume ya Taifa ya uchaguzi na kwamba wao
wanasubiri maelekezo ya Tume hiyo na daftari kamili litakalokuwa na
orodha ya wapiga kura wote litakalopelekwa kwenye vituo vya kupigia kura
kabla ya tarehe ya uchaguzi ili kutoa fursa kwa vyama vya siasa na
wananchi kupitia majina yote.