Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema mgawo wa umeme kwa sasa hauzuiliki nchini kutokana na mabwawa yanayotumika kuzalisha nishati hiyo nchini kukumbwa na ukame.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa uzalishaji wa umeme wa maji kwenye mabwawa hayo umeshuka hadi kufikia megawati 105 kutoka 561 kutokana na ukame unaoendelea majira haya ya kiangazi.
Mramba alisema hali hiyo imeilazimu Tanesco kutegemea kwa kiasi kikubwa umeme unaozalishwa na mitambo ya mafuta na gesi asilia hasa ile ya Kinyerezi I, ili kupunguza makali ya mgawo huo kwa kuwasha mtambo mmoja baada ya mwingine hadi mwishoni mwa Oktoba.
Alisema hadi kufikia jana, mabwawa yote makubwa yalikuwa na maji kidogo hivyo kushusha uzalishaji wa umeme kwa asilimia 81. 3.
“Bwawa la Mtera ambalo huzalisha megawati 80 kwa sasa halizalishi kwa kuwa hakuna maji, Kidatu lenye kuzalisha hadi megawati 204 kwa sasa linazalisha megawati 27 tu, Kihansi lenye uwezo wa juu wa kuzalisha megawati 180 linazalisha megawati 51. 5,” alisema Mramba.
Alisema hali kama hiyo ipo katika vyanzo vya maporomoko ya maji ya Pangani ambako uzalishaji umeshuka kutoka megawati 68 hadi 17, mtambo wa Hale kutoka 21 hadi 8, Bwawa la Nyumba ya Mungu kutoka 8 hadi 5. 5.
Mramba alisema mgawo huo pia unatokana na kushuka kwa kiwango cha uzalishaji gesi ya ya Songo Songo, ambako Kampuni ya Pan Africa inafanya ukarabati wa visima baada ya kubaini uzalishaji ulikuwa ukishuka kutoka megawati 340 hadi 260.
“Wananchi wawe watulivu mgawo huu hauna siasa hata chembe bali ni masuala ya kiufundi tu,” alisema Mramba.
Hata hivyo, alisema neema itaanza kuonekana leo kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao huenda makali ya mgawo wa umeme yakapungua baada ya mtambo mpya wa megawati 35 kuwashwa jana kwa kutumia bomba jipya la gesi.