Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ametaja mambo 13 atakayoyafanya ndani ya siku 100 iwapo atachaguliwa kuwa Rais, huku akisema “atawakata kilimilimi” wanaombeza kuwa hawezi kuondoa umaskini wa wananchi.
Lowassa alikuwa akihitimisha mikutano minne aliyofanya kwenye wilaya tatu za Jiji la Dar es Salaam jana kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe.
Wakati Lowassa akieleza hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alitangaza azimio la Kawe lililobeba ajenda kuu tatu, ikiwamo ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa mwongozo wa jinsi Serikali yake itakavyokabidhi madaraka kwa Ukawa kutokana na suala hilo kutokuwapo kikatiba, huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitangaza mkesha kwa wananchi siku ya kuamkia tarehe ya kupigakura na kutaka wanaume wabakie kulinda kura zisiibiwe.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya watu na viongozi wakuu wa Ukawa, Lowassa alisema mambo hayo atayatekeleza kwa kasi ya kilometa 120 kwa saa.
Lowassa aliyataja mambo hayo kuwa ni;
- Uhakika wa dawa na vifaa vya uzazi wa akinamama.
- Umeme wa uhakika nchi nzima.
- Kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
- Kuondoa kero kwa wafanyabiashara wadogowadogo na waendesha bodaboda.
- Kumaliza tatizo la maji nchi nzima.
- Mfumo bora na rafiki wa wafanyabishara wakubwa na wadogo.
- Kufuta ada na michango kwa wanafunzi.
- Kupunguza kodi ya mshahara kwa wafanyakazi.
- Kufuta kodi zote za mazao ya wakulima.
- Mkakati wa kukuza michezo na sanaa.
- Kuunda tume ya kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima.
- Kuanzisha kituo kila wilaya kwa ajili ya kutoa huduma za serikal.
- Kuboresha maslahi ya polisi, wanajeshi na walimu.
Mbali na mambo hayo 13, aliahidi kumaliza kilio cha wananchi cha kupata Katiba mpya inayotokana na maoni yao, akisema ni suala linalohitaji kutuliza kichwa kulipatia ufumbuzi.
“Umaskini si mpango wa Mungu,” alisema Lowassa ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu. “Nina hasira ya kupambana nao na kuwaondoa Watanzania katika umaskini.”
Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyeihama CCM mwishoni mwa mwezi Julai, aligoma kushuka jukwaani akitaka awekewe muziki acheze na maelfu ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza na kumkumbatia mkewe, Regina ambaye alifika uwanjani hapo wakati mkutano huo ukikaribia kumalizika, kisha akambusu.
Awali, Lowassa alisema idadi ya kura anazohitaji ili ashinde urais ni milioni 14.
Akiwa Mafinga mkoani Iringa, Lowassa aliomba wananchi wampigie kura milioni 10 ili awe Rais lakini jana alisema kuna haja ya kupata kura nyingi iwezekanavyo ili ushindi wake usiathiriwe.
“Kilichonileta hapa ni kuomba kura,” alisema Lowassa. “Naomba mnipigie kura milioni 14 na ushee ili ziweze kutosha kuwa Rais. Baada ya kupiga kura, wananchi mnatakiwa kuzilinda ili zisiibwe.”