Kijana Aliyesambaza Taarifa za Uongo Kuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Davis Mwamunyange Amelishwa Sumu Afikishwa Mahakamani - LEKULE

Breaking

10 Oct 2015

Kijana Aliyesambaza Taarifa za Uongo Kuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Davis Mwamunyange Amelishwa Sumu Afikishwa Mahakamani

Serikali jana ilimfikisha mahakamani bwana Bernedict Angelo Ngonyani kwa tuhuma za kutumia mtandao wa Facebook na WhatsApp kueneza taarifa za uongo kuwa mkuu wa majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange amelazwa Nairobi kwa madai ya kulishwa chakula chenye sumu.

Akizungumza kwenye eneo la mahakama ya kisutu jijini Dar es Salaam ambako mtuhumiwa huyo alifikishwa kwa ajili ya kusomewa mashitaka, wakili mkuu wa serikali Joanes Karungura alisema, mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo kwa kuvunja kifungu namba 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015.

Sheria hiyo ijulikanyo kwa lugha ya Kiingereza, Tanzania Cybercrime Act 2015, inakataza kusambaza ujumbe, taarifa au data za uongo au zisizothibitishwa kwa njia ya mtandao.

Ngonyani ambaye amenyimwa dhamana kutokana na aina ya kosa alilofanya la kuvunja sheria ya mtandao ya mwaka 2015 alikamatwa Septemba 25 mwaka huu kwa ushirikiano wa mamlaka ya mawasiliano nchini, Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Wakati huo huo serikali imewafikisha watuhumiwa watano katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, mmoja raia wa Afrika ya Kusini, mmoja raia wa China na watatu kutoka Pakstani, kwa kosa la kuiba kwa njia ya kimtandao wizi wenye thamani ya karibu shilingi billion moja, fedha za Kitanzania.

Mhandisi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini, TCRA anasema watuhumiwa hao walikutwa na laini zaidi ya mia moja zenye usajili bandia ambazo walikuwa wanazitumia kufanya biashara ya kupiga simu Kimataifa kinyume cha sheria
Mtuhumiwa wa makosa ya mtandao Benedict Angelo Ngonyani (24) (wa kwanza kulia) anayetuhumiwa kusambaza taarifa za uongo zinazomhusu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, akiwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu akisubiri kusomewa mashitaka. 

Wengine ni watuhumiwa wa wizi kwa kutumia mitandao ya simu (fraud and use of telecommunication network) Ally Hamze (53) raia wa Afrika Kusini (wa pili kulia), Huang Kun Bing (26) Raia wa China (wa tatu kulia) Irfan Mirza Baig (46) (wa kwanza kushoto) Hefeez Irfan (32) (wa pili kushoto) na Mirza Rizwan Baig (41) (wa tatu kushoto) wote watatu raia wa Pakistani wakiwa katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakisubiri kusomewa mashitaka ya wizi kwa kutumia mitandao ya simu (fraud and use of telecommunication network). 
 
Kesi zote zimeahirishwa hadi Oktoba 23 na watuhumiwa wote wamepelekwa rumande huku uchunguzi ukiendelea.



No comments: