Vijana wa Jeshi la Wananchi jana walivamia nyumba za wananchi waliokaribu na barabara kuu ya kutoka Mbeya kwenda Malawi katika wilaya ya Rungwe na kuwataka waamke kuondoa vizuizi vya moto, magogo na mawe vilivyokuwa kwenye barabara hiyo.
Kazi
hiyo ilifanywa baada ya vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Ukawa kuweka
vizuzi vya moto, magogo na mawe kwenye barabara hiyo ikiwa ni ishara
ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Rungwe.
Wanajeshi
walifika Kijiji cha Ndaga saa 4.00 usiku ambako waliyakuta magari
yakiwamo mabasi sita yaliyoshindwa kuendelea na safari ya kwenda Tukuyu,
Kyela na Malawi baada ya kuwekewa vizuizi.
Vijana
wa Jeshi la Wananchi waliamua kutembea kutoka Ndaga hadi Tukuyu
wakitoa vizuizi na kuwaamsha wananchi walio karibu na barabara ili
washiriki kazi hiyo huku wakitoa kichapo kwa waliokuwa wakichelewa
kuamka.
Waliopigwa ni pamoja na wagonjwa na wazee kadhaa wakiwamo wachungaji ambao walikutwa wamelala usiku huo.
Kiongozi
mmoja wa Kijiji cha Katumba ambaye aliomba jina lihifadhiwe alisema
hatua ya jeshi ilitokea baada ya vijana wanaodaiwa kutoka Mbozi,Tunduma
na Mbeya mjini wakishirikiana na wafuasi wa Ukawa kufanya vurugu tangu
saa 10,00 jioni ya juzi baada ya kutangazwa matokeo ya ubunge katika
Jimbo la Rungwe.
Naye
mkazi wa Kijiji cha Kiwira Tujobe Mwakipu alisema vijana hao
walifanya vurugu bila kuzuiwa na wanasiasa waliogombea ubunge.
Alisema
vurugu zilianza baada ya kutangazwa matokeo ya Ubunge ambayo yalimpa
ushindi mgombea wa CCM, Saul Amon kwa kura 47,862 akimshinda mpinzani
wake wa karibu, John Mwambigija aliyepata kura 43,613.
Alisema
vurugu zilianzia Tukuyu mjini ambako vijana walikusanyika kudai matokeo
na yalipotangazwa hawakuridhika na kuanza kuchoma barabara kuanzia saa
10 ya jioni.
Akizungumzia
yaliyowakuta wazee ,John Mwampi wa Kijiji cha Ntokela alisema usiku
wa kuamkia jana wananchi wengi walipigwa na wanajeshi waliovamia nyumba
zao kuanzia saa 7.00 usiku hadi 12.00 asubuhi walipomaliza kazi ya
kuondoa vizuizi kwenye barabara kuu hiyo maeneo ya Ndaga, Ntokela,
Kiwira, KK, Mwabegele na Katumba.
Mwampi
alisema wanajeshi walifika eneo la KK saa 10.30 na kuwaamsha kwa bakora
wananchi wenye nyumba zilizo karibu na barabara huku wakiwataka wakatoe
mawe, magogo na moto uliokuwa ukiwaka katikati ya barabara.
Naye
Mchungaji Yesaya Kilindu wa kitongoji cha Ntupwa katika Kijiji cha KK
wilayani Rungwe alisema wanajeshi waliingia kwenye nyumba yake saa 10.00
usiku na kuanza kuwatandika bakora huku wakiwaamuru wakaondoe mawe na
magogo kwenye barabara kuu.
‘’Walituchapa sisi na pia walikwenda nyumba ya Mwalimu chaula ambako waliwapiga na kuiba simu yenye tamani ya Sh200,000’’, alisema na kufafanua kwamba tukio hilo lilikuwa baya.
Kaimu
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Moses Mashaka alipoulizwa alisema kamati ya
usalama ya wilaya ilikuwa ikiendelea kufuatilia nyenendo za vijana na
kwamba haikuwa na taarifa za kutoa kwa vyombo vya habari.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa Ahmed Msangi alipoulizwa alisema polisi
waliwadhibiti vijana waliofanya vurugu na kuwakamata kadhaa, lakini
alisita kuzungumzia zaidi akisema bado wanawasaka wengine.
No comments:
Post a Comment