MARA
kadhaa linapoibuka suala la kugawana mali pale ndoa
inapohesabika kushindikana masuala kadhaa ya msingi na
yanayohitaji uelewa huwa yanaibuka. Moja ya suala kati ya
masuala ambayo huibuka ni hili la kutenganisha na kufafanua
hadhi ya mali za wanandoa ili mgawanyo uweze kufanyika kwa
haki. Yawezekana mwanandoa akadhani ana haki katika mali fulani
lakini kumbe kisheria hana haki hiyo ni mtazamo wake ndio
unamsukuma kuamini hivyo.
Halikadhalika yawezekana mwanandoa kudhani hana haki katika mali fulani kumbe anayo haki. Ili kujua una haki ipi katika mali ipi na huna haki katika mali ipi yahitajika kujua misingi ya kisheria inayotumika kugawanya mali za wanandoa.
Halikadhalika yawezekana mwanandoa kudhani hana haki katika mali fulani kumbe anayo haki. Ili kujua una haki ipi katika mali ipi na huna haki katika mali ipi yahitajika kujua misingi ya kisheria inayotumika kugawanya mali za wanandoa.
1.KUGAWANA MALI ZA WANANDOA.
Ieleweke
kuwa tunapoongelea wanandoa kugawana mali tunaongelea talaka.
Hakuna kugawana mali bila talaka. Na kisheria talaka inapotoka
tu swali linalofuata ni habari ya mali na watoto kama wapo.
Mali si lazima magari na manyumba lakini pia hata vyombo vya
ndani vikiwemo vitanda, makabati, sahani n,k nazo ni mali kwa
mujibu wa sheria. Navyo huhitaji mgao.
2. JE KUGAWANA MALI NI NUSU KWA NUSU ?.
Linapokuja
suala la kugawana mali wengi hudhani mtindo unaotumika kugawa ni
ule wa nusu kwa nusu. Jambo hili si kweli kwakuwa sheria
ya ndoa 1971 iliyofanyiwa marekebisho 2002 haisemi kuwa
utaratibu wa kugawana mali ni nusu kwa nusu. Sheria hii imeweka
msingi mkuu wa kugawana mali ambao ndio hutumika katika
mahakama zetu katika kutoa maagizo ya kugawa mali za
wanandoa.
Msingi
uliowekwa na sheria ni msingi wa kiwango cha mchango wa
mwanandoa katika kupatikana kwa mali husika. Kiwango
alichochangia mwanandoa katika kupatikana kwa mali hiyo ndicho
kitakachokadiriwa na kiwango hicho ndicho atakachopewa. Kwa hiyo
kama ni nyumba ya vyumba sita mmoja anaweza kupata chumba
kimoja na mwingine akapata vitano kutegemea na mchango wake. Na
mchango hapa sio leta ni lete. Mchango sio hela tu hata kazi
za nyumbani anazofanya mama wa nyumbani ambaye haleti hela
nazo huitwa mchango ambapo hukadiriwa na kupata kile
anachostahili.
3. MALI KABLA YA NDOA NA BAADA YA NDOA.
Katika
kutenganisha mali za wanandoa huwa zinatenganishwa katika
makundi makuu matatu. Kwanza kuna mali ambazo mtu alikuwa nazo
kabla ya ndoa na wakati anaingia katika ndoa ameingia nazo.
Kwa mfano mwanamke ameolewa akamkuta mwanaume tayari ana nyumba
yake. Pili kuna mali ambazo zimepatikama wakati wawili wakiwa
katika ndoa . Kwa mfano ndoa imefungwa wawili wakaanza kuishi
pamoja na taratibu wakaanza kujenga na kukamilisha. Na tatu ni
mali ambazo zimepatikana katika ndoa lakini zikiwa hazina
uhusiano wowote wa kindoa kwa mfano kurithi au kuzawadiwa mali.
Tutaona hapa chini mazingatio ya sheria ya kila moja katika
haya.
4. JE MALI ILIYOPATIKANA KABLA YA NDOA INAHESABIKA NI YA FAMILIA.
Mali
iliyopatikana kabla ya ndoa na ikaendelea kuwepo kipindi cha
ndoa inaendelea kuwa ya huyo mwenye nayo bila ushirika wa
mwenza wake. Kama ni nyumba mwanamke alikuwa nayo kabla ya
kuolewa au ni mwanaume alikuwa nayo kabla ya kuoa basi
inaendelea kuwa ya kwake peke yake na haihusiki katika mgao
suala la mgao linapojitokeza.
Hata
hivyo inaweza kuingizwa katika mgao ikiwa kuna mchango wowote
wa kuiendeleza uliotolewa na mwenza. Kwa mfano kabla ya ndoa
ilikuwa na vyumba viwili lakini katika kipindi cha ndoa
imepanuliwa na kufikia vyumba vitano, au ilikuwa haina uzio, au
haina madirisha kabla ya ndoa lakini baadae vitu hivi
vikawepo. Katika hali kama hiyo itatakiwa iingizwe katika mgao
na kutazama kiwango cha mchango wa kila mmoja katika uendelezaji
huo. Ni hapo ambapo mchanganuo utafanyika ili kila mmoja apate
haki kutokana na kiwango cha mchango wake.
Ikiwa
hakuna uendelezaji wowote uliofanyika katika mali yaani labda
nyumba ilivyokuwa kabla ya ndoa ndivyo hivyohivyo ilivyoendelea
kubaki hata baada ya ndoa basi mali hiyo haitatakiwa kuingizwa
katika mali za mgao bali itabaki mali ya mwanandoa mmoja
pekee ambaye ndiye mmiliki wa tangu awali.
Hali
ni hiyo hiyo hata kwa mali ambayo imepatikana katika ndoa
lakini ikiwa haina uhusiano na kipato cha wanandoa, kwa mfano
mali ya urithi au zawadi. Hii ina maana ikiwa mali hii
itaendelezwa basi mchango wa uendelezaji utatathiminiwa na ikiwa
haitaendelezwa basi itabaki mali ya mrithi au mpewa zawadi
pekee na haitahusu mgao.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment