ISOME HAPA SAFARI NZIMA YA MAISHA YA MAREHEMU MCH.MTIKILA - LEKULE

Breaking

5 Oct 2015

ISOME HAPA SAFARI NZIMA YA MAISHA YA MAREHEMU MCH.MTIKILA


MCHUNGAJI Christopher Mtikila ni Mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP) ambacho kina usajili wa kudumu hapa nchini. 

Mtikila alizaliwa mwaka 1950 mkoani Iringa, kusini mwa nchi yetu.
(Kwa bahati mbaya, hadi nachapisha uchambuzi huu sikupata taarifa za elimu yake) kwani hakuwa mwepesi kutoa ushirikiano mwezi mmoja uliopita alisafiri kwenda nje ya nchi na kurejea wakati nikiwa katika hatua za mwisho za uhariri.

Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa kanisa la Kipentekoste la Full Salvation Church. Lakini pia kwa muda mkubwa wa maisha yake amekuwa anajihusisha sana na harakati za haki za binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo kiitwacho “Liberty Desk”. 

Kanisa lake ni moja ya makanisa machache sana hapa Tanzania yenye vitengo vya namna hiyo.
Umaarufu wa Mtikila ulikua sana mwanzono mwa miaka ya 1990 kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu kile anachokiita “uhujumu wa uchumi unaofanywa na wahindi” (ambao anawaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za Tanzania,ni kati ya mambo machache yaliyofanya asikike kila kona ya nchi.

Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar, alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na sio Tanzania. 

Hata hivyo Mtikila ilimpasa abadili msimamo wake katika miaka ya hivi karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama toka Zanzibar (kama sheria ya uchaguzi inavyotaka) na hivyo chama chake kilipata usajili wa kudumu.
 
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba. 

Mwaka 2004 pia alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala. Kwa ujumla maisha yake yamekuwa ni ya harakati muda wote, akipambana awezavyo, akisimama kidete inavyowekana na akijikuta matatani kila uchwao. Mchungaji Mtikila amemuoa Bi. Georgia na wana watoto.



MBIO ZA UBUNGE
Mwaka 1997, Mbunge wa jimbo la Ludewa kwa tiketi ya CCM, Horace Kolimba aliitwa na Kamati Kuu ya chama chake mjini Dodoma kwenda kujibu mashtaka ya ndani ya chama juu ya kauli ambazo alikuwa akizitoa kwamba “CCM imepoteza mwelekeo”, baadhi ya viongozi wa chama chake walimchukulia kama msaliti na wengine wakimuona kama mtu aliyethubutu kusema ukweli bila kumuhofia Nyerere.

 Hata hivyo Kolimba alifariki hukohuko Dodoma katika siku ambazo alikuwa akihojiwa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipotangaza kukuwepo kwa uchaguzi mdogo, ndipo Mchungaji Christopher Mtikila, alikihama chama chake cha DP akajiunga CHADEMA na kuomba ridhaa ya kugombea jimbo la Ludewa, Chadema ikampa ruhusa hiyo. 

Mtikila ni mzaliwa wa Ludewa na alifanya hivyo kwa sababu chama chake cha DP kilikuwa kimenyimwa usajili.


Uchaguzi wa Marudio ulifanyika tarehe 25 Mei 1997 na kumpa ushindi mgombea wa CCM Prof. Chrispin Haule Che Mponda. Prof Mponda alipata kura 20,111 dhidi ya kura 8,386 za Mchungaji Christopher Mtikila wa CHADEMA. Mgombea wa NCCR ambayo haikuwa imejijenga vilivyo Ludewa, Barnabas Kidulile, alipata kura 1,271.
Hata hivyo, baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mchungaji Mtikila alisikika akihitilafiana na CHADEMA hadharani huku akiipa shutuma nzito nzito, akafukuzwa kwenye chama hicho na ndipo akaendelea kuwekeza nguvu kwenye mipango ya kukamilisha usajili wa chama chake.

MBIO ZA URAIS
Mtikila alianza rasmi harakati za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya DP alikuwa kati ya wagombea 10 wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. 

Katika uchaguzi huo alipata kura asilimia 0.27 ya kura zote, akiwa nyuma ya Jakaya Kikwete wa CCM (asilimia 80.28), Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF (asilimia 11.68), Freeman Mbowe wa CHADEMA (asilimia 5.88), Augustine Mrema wa TLP (asilimia 0.75) na Dkt. Sengondo Mvungi wa NCCR (asilimia 0.49).

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Mtikila hakugombea nafasi ya Urais na chama chake hakikuweka mgombea na kwa mwaka huu 2015 hajaweka msimamo wake wazi japokuwa taarifa za ndani ya chama hicho zinaonesha kuwa kinaweza kusimamisha mgombea na mtu huyo akawa ni Mtikila.

Nimemuweka katika Orodha hii kwa sababu tayari anatajwa kuwa na sifa,vigezo na hata historia ya mapambano inayompa nafasi ya kuweza kusimama mbele ya watanzania kuomba uongozi wa juu.

NGUVU YAKE 
Jambo la kwanza ambalo bila shaka linampa Mtikila nguvu ikiwa ataingia kwenye kinyang’anyiro cha urais ni umaarufu wake. Mtikila ni maarufu sana, si kwa watu wenye umri wa zamani tu, lakini pia hata kwa vijana wadogo wa sasa. 

Ni vigumu sana kama mtanzania yeyote anafuatilia masuala ya siasa katika nchi au anafuatilia habari mara kwa mara na asimjue Mtikila. Ni kiongozi anayejishughulisha na mambo mengi mno na harakati zilizopitiliza na kwa mwanasiasa anayetaka nafasi ya juu, umaarufu unaweza kuwa karata muhimu, la msingi tu umaarufu huo vichwani mwa watu uwe na maana ya kumuona kama “mtu muhimu” katika hatua zake.

Lakini jambo la pili linalompa nguvu na sifa zaidi, ni kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya mara kwa mara, ya kufungua kesi za masuala ambayo serikali inakuwa imewanyima raia kwa muda mrefu. Mara nyingi katika siasa za Afrika, kesi za kuishtaki serikali kwa masula ambayo yanaonekana kuwa makubwa huwa linaonekana kama jambo hatari hata kwa usalama wa mhusika, Mtikila.

Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali toka kwa Mkuu wa Wilaya na polisi n.k. Hebu tujiulize, ni vyama vingapi vya siasa vimewahi kuwa na “uthubutu” huo? 

Mtikila alishinda kesi ya mgombea binafsi na aliiweka serikalini kwenye njia panda kwa asilimia mia moja. Katika suala hili yeye ni mtu wa kujivunia sana na kama upiganaji wa kiwango hiki peke yake ndiyo ungekuwa tiketi ya urais basi Mtikila tayari angestahili tuzo hiyo bila mjadala. Hakuna mwanasiasa mwingine yeyote hapa Tanzania aliyewahi kupambana na serikali mahakamani kila kukicha kama Mtikila, hayupo!

Lakini jambo la tatu linalompa nguvu na sifa ni ni Misimamo ya kipekee. Mtikila hajali anapokuwa ana ajenda zake na misimamo yake na mara nyingi misimamo hiyo huwa ni ya kipekee hata kama ni mibaya kiasi gani, yeye huisimamia na kubakia nayo hata kama wenzake wote mtamkimbia. 

Nakumbuka tulipokuwa Bunge Maalum la Katiba, Mtikila alikuwa na ajenda ya kusimamisha bunge lile lisifanye kazi kwa sababu limeanza kinyume na sheria na halina hadi ya kutunga katiba ya nchi. Pamoja na wanasheria wakongwe sana kuwa na mawazo tofauti naye, bado alishikilia msimamo wake na aliondoka kwenda Dar Es Salaam kwa minajili ya kufungua kesi husika (sina taarifa jambo hili lilipoishia).

Na hata baadaye, vyama vinavyounda UKAWA vilipoamua kutonoka Bungeni, Mtikila aliunga mkono uamuzi huo na alisisitiza kuwa yeye anafanya kazi na umoja huo kwa suala la katiba, sijapata taarifa za hatma yake katika kuendelea kuwa ndani ya UKAWA, lakini nachojua ni kwamba misimamo hii ya Mtikila kuna wakati imekuwa na tija kubwa sana, si kwake tu bali kwa taifa zima. 

UDHAIFU WAKE
Udhaifu wa kwanza wa Mtikila ni utoaji wa “Kauli tata” ambazo kuna nyakati zinaudhi na kuamsha hasira ya upande uliotuhumiwa. Mtikila ana tabia ya kuongea mambo magumu na mkishindana sana akakudharau huweza kukuita jina baya sana ambalo hukuwahi kufikiri kuwa unaweza kuitwa au kupewa. 

Mara kadhaa amewahi kusikika akitoa shutuma kali sana kwa viongozi wa nchi, vyama vya upinzani n.k. Sifa hii ya Mtikila si sifa sahihi sana kwa mtu ambaye ana ndoto au anaotewa ndoto za kushika uongozi wa juu wanchi siku moja.

Lakini jambo la pili ambalo naliona kama udhaifu pia, Mtikila hupenda kushughulikia mambo ya hatari peke yake na wakati mwingine bila kufanya kazi ya kutosha kuwaelimisha wananchi na vyombo vya habari na kutafuta hali ya kupewa uzito na mioyo ya wananchi na wadau. 

Tabia hii ya Mtikila ya kuamka na ajenda nzito mkononi na kulazimisha ajenda anayotoa iungwe mkono ghafla bila kuwaandaa wananchi, siyo jambo zuri kisiasa. 

Kuna masuala ya msingi sana anayapigania na yanapotoshwa na vyombo vya habari, na wanasiasa wa vyama vingine n.k kwa sababu tu hakufanya kazi ya siasa ya kuyatangaza masuala hayo, kuomba ushirikiano wa wenzake n.k. Ili uwe kiongozi mzuri una wajibu wa kuwashirikisha watu waliokuzunguka maamuzi makubwa unayotaka kuyafanya ili uungwe mkono. Kujifanyia peke yako kunakuwa hakuna tija kubwa kwa maslahi mapana ya wote.

Na mwisho, Mtikila amekuwa akitoa kauli zinazodhaniwa kuwa ni za kibaguzi sana na hili haliko “uvunguni”, amefanya hivyo mara nyingi mno katika mikutano yake na hata mbele ya vyombo vya habari. 

Kuna wakati amekuwa akisikika hadharani akiwatuhumu Wahindi kwa lugha za kibaguzi sana, anawaita “Magabacholi”, lakini pia kuna wakati amewahi kulalamikiwa hata na nchi jirani ya Rwanda kwa namna alivyowahi kuyashutumu makabila makubwa ya nchi hiyo kwa kauli za kibaguzi. 


Kiongozi mmoja wa juu wa Serikali nimewahi kumsikia akisema kuwa alipokutana na Rais Kagame wa Rwanda, baada ya salamu Kagame akamuuliza kiongozi huyo “Who is Reverend Mtikila”? (Mchungaji Mtikila ni nani?). Mtikila siyo tu kuwa alikua anaipa chemsha bongo Serikali hapa ndani, hata huko nje ya nchi wanaumiza vichwa juu yake na hili siyo suala la kujivunia sana kama kweli nchi inatafuta viongozi watakaoimarisha uhusiano na nchi za jirani.