CHADEMA Wamshitaki Rais Kikwete UN, AU na Katika Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) - LEKULE

Breaking

20 Oct 2015

CHADEMA Wamshitaki Rais Kikwete UN, AU na Katika Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC)



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimemshitaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari  jana mchana ukumbi wa Kisenga uliopo Millenium Tower, wakili wa Chadema, John Mallya alisema Rais  Kikwete ameshitakiwa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Mahakama ya kihalifu Uholanzi kwa sababu anatumia madaraka yake vibaya kutisha wananchi kuelekea uchaguzi mkuu.

Mallya alisema kuwa Mashitaka hayo yameelekezwa Umoja wa Mataifa lakini pia nakala za tuhuma dhidi ya Rais Kikwete zimepelekwa pia Umoja wa Afrika (AU) na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita iliyopo The Hegue Uholanzi.

Kwa mujibu wa wakili huyo wa Chadema, barua hiyo ya tuhuma dhidi ya Rais Kikwete imesainiwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Prof. Abdallah Safari.

Mashataka haya yanakuja ikiwa ni miezi miwili tangu Rais Kikwete ailaumu  Mahakama hiyo ya kihalifu kwa kusema kuwa viongozi wa Afrika hawafurahii kwa namna ambavyo mahakama hiyo inavyofanya kazi zake kwa kuwashughulikia zaidi viongozi wa mataifa ya Afrika.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete aliitoa jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa 16 wa Umoja wa Wanasheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika-SADC,

Hiyo ilikuwa ni siku moja baada ya ICC kueleza kwamba inafuatilia mwenendo wa uchaguzi nchini Tanzania.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, alikaririwa na vyombo vya habari vya Aljazeera na Gambia Today akisema kuwa Mahakama hiyo inatazama kwa umakini mkubwa yanayotokea Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu kama ilivyofanya katika nchi za Kenya, Ivory Coast na Congo na kwamba itachukua hatua za haraka kama kutakuwa na uvunjaji wa haki za binadamu.

Kauli hiyo ya Bensouda ilitanguliwa na ile iliyotolewa na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Lowassa alilazimika kusema hayo katika ziara ya kutafuta wadhamini katika mikoa ya Arusha na Mwanza  kwa  kulitahadharisha Jeshi la Polisi juu ya uwepo wa Mahakama ya ICC kutokana na kitendo chake cha kutumia nguvu dhidi ya wapinzani kwa kuupiga mabomu msafara wake.

No comments: