Baadhi
ya Ujumbe wa Tanzania na Ujumbe wa Japan wakiwa kwenye majadiliano.
Katikati ni Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius
Likwelile, kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar Bw.
Khamis Mussa na Kamishna wa Fedha za Nje Bw. Said Magonya na kulia kwake
ni Rais wa JICA Bw. Hiroshi Kato. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile wa kwanza kulia akiendelea kufanya majadiliano na ujumbe wa JICA ukiongozwa na Rais wa JICA Bw. Hiroshi Kato wa pili kulia.
Ujumbe wa Tanzania na Ujumbe wa JICA wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile wakati wa majadiliano
ya kuwekeza katika sekta ya umeme, utalii na kuboresha mazingira ya
biashara.
JAPANI
YAKUBALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA KUCHANGIA BAJETI YA
MAENDELEO KATIKA MIKUTANO YA WB & IMF HAPA NCHINI PERU - LIMA
Serikali
ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania yapata dola milioni 280 kutoka Benki
ya Dunia na Japani, fedha hizo zitatumika kusaidia mipango mbalimbali
nchini Tanzania. Akiongea na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia ukanda wa
Afrika Bw. Makhtar Diop na Rais wa Shirika la Maendeleo ya Japan-JICA
Bw. Hiroshi Kuto, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa
Serikali Dkt. Servacius Likwelile alisema dola milioni 230 zimetolewa
na Benki ya Dunia. Kiasi cha Dola milioni 100 ni kwa ajili ya kuhimiza
mambo ya uwazi katika utawala, dola milioni 80 ni kwa ajili ya kuboresha
mazingira ya kufanya biashara na dola milioni 50 ni kwa ajili ya
kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii yaani pensheni.
Shirika
la Maendeleo la Japan (JICA) wamethibitisha kuendelea kuunga mkono
Serikali ya Tanzania katika mipango ya maendeleo. Wakiwa katika kikao
na ujumbe kutoka Tanzania, Bw. Hiroshi Kato ambaye ni Makamu wa Rais wa
shirika hilo alisema kuwa , Serikali ya Japan kupitia shirika lao la
maendeleo ( JICA) lina mipango ya kuunga mkono Tanzania na Kenya
watajenga barabara ambayo itaunganisha Arusha na Mombasa kwa kiwango
cha juu ili kuweza kurahisisha mazingira ya biashara na utalii. Bw. Kato
katika mazungumzo yake aliongeza kuwa bado wao wako tayari kusaidia
kupitia bajeti kuu ya Serikali kama vile ambavyo wamekuwa
wakifanya miaka ya nyuma.
Akifafanua
kuhusiana na sekta ya hifadhi ya jamii Dkt. Likwelile alisema kuwa
uboreshaji wa pension umeahirishwa kwa sasa na wameomba Shirika la kazi
la Kimataifa (ILO) wafanye mapitio ya sekta hiyo na baada ya mapitio
hayo ndio tutajua ni masuala gani tunaweza kuyazingatia ili kuboresha
sekta yetu ya hifadhi ya jamii.
Katika
majadiliano na viongozi wa benki ya Dunia Dkt. Lilkwelile aliwaeleza
kuwa, Tanzania kuna changamoto kubwa kwasababu uzalishaji wa umeme
kupitia maji umepungua kutokana na kina cha maji kupungua katika maeneo
ya uzalishaji hivyo tunategemea gesi.
“Tunategemea
gesi ya Kinyerezi One ambayo inatupatia megawatts 405-407, na vilevile
tunapata umeme kutokana na matumizi ya mafuta ambapo ni gharama kubwa na
uzalishaji haujafikia lengo ambalo ni mahitaji yetu ya siku ambayo
tunapata. Tuna mapungufu ya megawatts160, suala hili limeleta shida
sana kwenye bajeti yetu”. Alisisitiza Likwelile
Benki
ya Dunia watashirikiana na Idara ya Serikali ya Uingereza ya maendeleo
ya Kimataifa (DFID) pamoja na Japan kuwekeza katika reli ya kati ili
kuunga mkono jitihada zetu za kuboresha huduma ya reli nchini Tanzania,
Likwelile aliendelea kufafanua.
Kwa
upande wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania ni kwamba uchumi bado unakuwa
kati ya asilimia 6.5 mpaka 7, mfumuko wa bei umeshuka japokuwa unapanda
kidogo kufikia asilimia 6.4, akiba ya fedha za kigeni bado inawezesha
Tanzania kuingiza bidhaa za karibu miezi minne, aliongeza Dkt.
Likwelile.
Katika
majadiliano hayo Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Bw. Diop
alisisitiza kuwa Tanzania iweke msisitizo mkubwa kwenye kilimo chenye
tija na cha kibiashara pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu ambayo
itasaidia uchumi kuimarika hasa kwenye nishati, reli, barabara,
mawasiliano pamoja na kuwekeza kwa vijana kwani ni wengi sana
na wanahitaji uhakika wa kupata ajira. Tukiweza kufanya kilimo kikawa
cha tija na kuwekeza kwenye viwanda vidogovidogo na kuwapa vijana elimu
ambayo itawasaidia kuweza kujitegemea, Tanzania itaweza kusonga mbela.
Akiendelea
kufafanua Bw. Diop alisema, kutokana na uchumi wa Tanzania ulivyo
hakuna sababu ya kukusanya mapato yetu ya kodi kwa kiwango cha sasa,
tuna uwezo wa kwenda hadi asilimia 12 ya pato la Taifa. Naye Dkt.
Likwelile alimuhakikishia Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Bw.
Diop kuwa lengo la Tanzania ni hili ila tunahitaji uwekezaji ili tuweze
kufikia lengo tuulilokusudia, maana tumeweka ukomo wa fedha angalau
tufikie mpaka asilimia14.5 lakini tunaweza kwenda mpaka asilimia 17 – 20
katika miaka mitatu ijayo.
Katika
kuhitimisha majadiliano hayo Dkt. Likwelile alisema kwamba ushirikiano
kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni mzuri na mkubwa sana. Kiwango cha
fedha ambacho tunakipata kutoka kwao kinazidi kuongezeka na wameweza
kuturuhusu kuwekeza kutumia mlango mwingine mfano kwenye Chama cha
Maendeleo ya Kimataifa(IDA) na pia kwa sasa tumeweza kupata fedha
kupitia Benki ya Kimataifa ya ujenzi na maendeleo(IBRD) kwa ajili ya
upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.
Hali ya hewa mjini hapa ni baridi sana.
Imetolewa na: Bi. Ingiahedi Mduma
Msemaji wa Wizara ya Fedha
Peru – Lima
No comments:
Post a Comment