Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kada wa CCM, Balozi Juma Mwapachu leo amerudisha kadi ya uanachama katika ofisi za CCM Kata ya Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Amesema anajiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 atatangaza chama anachojiunga miongoni mwa Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda umoja huo.
Mwapachu amesema haoni sababu ya kutaja chama hicho sasa kwa vile lililo muhimu kwao hivi sasa ni umoja miongoni mwa wanamabadiliko na kujipambanua katika imani ya chama cha siasa hakuwezi kuwa na tija kwa umoja huo.
Amesema Lowassa anakwenda kuwa Rais wa Wanaukawa wote, hivyo watu wote wanaoamini katika mabadiliko ndani ya vyama hivyo wanapaswa kuwa wamoja kwa kuuwezesha umoja huo kuibuka na ushindi.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mtaa wa Mikocheni A, Sudi Odemba amesema chama chake hakitapata madhara yoyote kutokana na hatua ya Balozi Mwapachu kijiengua na kutangaza kujiunga Ukawa.
Amesema Mwapachu hakuwa mwanachama aliyejitoa kukisaidia chama katika siku za karibuni na kwamba hajawahi kushiriki mikakati thabiti ya kukipatia CCM ushindi katika ngazi ya mtaa japo chama hicho kiliweza kuibuka na ushindi wa kishindo.
No comments:
Post a Comment