Mwandishi wa makala hii ni Ananilea Nkya ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa TAMWA.
******
Watu wanaokampeni kushawishi Watanzania wamchague John Magufuli kuwa Rais wa tano wa Tanzania kwa kutumia kigezo cha uadilifu wanadhani ataweza kuzuia serikali ya CCM kuwa fisadi na hivyo umaskini wa wananchi kupungua.
Kimsingi wanajidanganya maana Magufuli akichaguliwa ufisadi wa kimfumo unaofanywa na serikali ya CCM ili chama hicho kibaki madarakani utaendelea kwa kasi na hivyo pengo kati ya watawala wachache kutajirika kufuru na mamilioni ya wananchi maskini wa kutupa litaongezeka mara dufu.
Nchi yetu ilipopata uhuru maadui wa ustawi wa wananchi walikuwa ni watatu—adui mkuu ujinga— na adui wengine wawili wanaotokana na ujinga—adui umaskini na adui maradhi.
Lakini katika zama hizi za utandawazi na demokrasia ya vyama vingi vya siasa ameongezeka adui mwingine hatari nchini kwetu–adui ufisadi.
Ufisadi ameshamiri nchini baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanza mwaka 1992.
Chanzo cha ufisadi nchini ni CCM kung’ang’ania madaraka kwa kutumia nguvu ya fedha na hivyo serikali yake kila inapochaguliwa hugeuka kuwa fisadi na kuiba fedha na mali za umma.
Hivyo, ikitokea Magufuli akichaguliwa wananchi wengi wataendelea kuwa maskini kwa sababu inaelekea Magufuli mwenyewe au hajui au haamini kwamba chanzo cha umaskini nchini ni serikali ya CCM kuwa fisadi na kuendekeza rushwa, ubabe, giliba, uongo na siasa za maji taka kushinda uchaguzi.
Inaelekea Magufuli hajatambua kuwa kuzuia ufisadi unaozaa mafuriko ya wananchi maskini Tanzania kunahitaji nchi iweke misingi ya kikatiba, lakini CCM kwa kukataa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi isiandikwe 2014 iliikataa misingi hiyo kwa sababu kinajua kinanufaika na udhaifu wa kikatiba uliopo sasa.
CCM inachofanya sasa ni Magufuli kuwapumbaza wananchi kwamba eti baada ya yeye kuteuliwa kugombea Urais kwa tiketi ya CCM, mafisadi wameanza kuikimbia CCM.
Magufuli anataka kuwaaminisha Watanzania kuwa umaskini unakabili mamilioni ya Watanzania umesababishwa na wanaCCM walioondoka kwenye chama hicho baada ya yeye kuteuliwa kugombea Urais!
Pengine ndiyo sababu Magufuli anaahidi kwenye kampeni zake kwamba akichaguliwa Rais ataanzisha mahakama ya mafisadi kama alivyokaririwa kwenye mikutano yake ya kampeni huko Dodoma.
Ninanukuu: ‘’Baadhi ya mafisadi wezi wameanza kukimbia baada ya CCM kuniteua mgombea urais lakini nikiingia Ikulu, nitawafuata huko waliko ili niwashughulikie vizuri ndiyo maana nimesema nitaunda mahakama ya mafisadi’’
Wananchi wanajiuliza kama ufisadi wa fedha na mali za nchi unafanywa na serikali inayopewa dhamana ya kuwa mlinzi wa fedha na mali za Watanzania endapo Magufuli atachaguliwa na serikali yake kuunda mahakama ya mafisadi, je majaji wa mahakama hiyo watapata wapi ujasiri wa kumtia hatiani fisadi mkuu (serikali) wakati kiongozi mkuu wa serikali (Magufuli) ndiye atakuwa amewateua majaji wa mahakama hiyo? Je serikali inaweza kujihukumu yenyewe?
Aidha wananchi wanajiuliza je serikali ya CCM imekuwa ikishindwa kuchukua hatua za kisheria kudhibiti ufisadi wa fedha na mali za umma unaofanywa na serikali ya kwa vile nchi haina mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi au ni kwa vile chama chao ni mnufaika wa ufisadi?
Wananchi wanauliza swali hili kwa sababu ipo mifano mingi kuonyesha serikali ya CCM ni fisadi .
Mfano wa kwanza: Ufisadi wa EPA kuiba kwenye Akaunti ya EPA benki kuu jumla ya shilingi bilioni 133 mwaka 2005/6. Wananchi walishangaa kuona Rais wa Jamhuri yetu alivyopata kigugumizi kwenye ufisadi huo.
Wananchi wanajiuliza ilikuwaje mlinzi mkuu (serikali ya CCM) kama kweli haikunufaika na ufisadi wa EPA haikuchukizwa na kitendo hicho cha aibu na kuchukua hatu za kisheria?
Kadhalika wananchi wanajiuliza, kama kweli wizi huo wa EPA haukuhusisha serikali yenyewe kunufaisha CCM ni kwa nini serikali ya CCM ilisema waliokwapua fedha hizo wamepewa muda wa kuzirejesha benki na hadi leo (miaka 10 baadaye) haijawatangazia Watanzania hatma ya fedha hizo?
Mfano wa pili: Ufisadi wa Richmond. Kukotana na ukosefu wa umeme nchini serikali ya CCM iliingia mkataba na kampuni ya kigeni Richmond ili nchi ipate umeme.
Kabla kampuni hiyo kuanza kuzalisha umeme zilitoka tuhuma kwamba Richmond ilikuwa ni kampuni feki.
Wakati huo Edward Lowassa alikuwa Waziri Mkuu, kimamlaka hakuwa Waziri wa Nishati, lakini aliamua kujiuzulu kulinda heshima ya serikali.
Lakini cha kushangaza baada ya kujiuzulu Lowassa kampuni ya Dowans iliyoirithi Richmond iliendelea kulipwa fedha nyingi kila mwezi hadi zikafikia bilioni 172.
Wananchi wanajiuliza kama CCM ilikuwa hainufaiki na mabilioni hayo yaliyokuwa yanalipwa Dowans na kwamba mnufaika wa ufisadi huo alikuwa ni Lowassa ni kwa nini Dowans waliendelea kulipwa baada ya Lowassa kuachia ngazi? Ni kwa nini Lowassa hajafikishwa mahakamani hadi leo kama tuhuma dhidi yake zina ushahidi?
Wananchi wanajiuliza kama CCM na serikali yake wanajinasibu ni walinzi waaminifu wa mali na rasilimali za Tanzania na kwamba wanastahili kuendelea kuajiriwa kuwa mlinzi mkuu wa fedha na mali za Tanzania baada ya uchaguzi tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015 ni kwa nini serikali ya CCM ilipata kigugumizi kumpeleka Lowassa mahakamani kumdai alipe hizo shilingi bilioni 172 kama kweli ndiye aliyenufaika na ufisadi huo?
Mfano wa tatu: Ufisadi wa kuuza kwa bei chee nyumba za Watanzania zenye thamani ya mabilioni ya shilingi huku leo hii serikali ikitumia fedha nyingi za umma kuwapangishia makazi hotelini watawala.
Wananchi wanafahamu kuwa msimamizi wa uuzwaji wa nyumba hizo ulifanyika wakati Magufuli akiwa na Waziri nyumba na makazi.
Karibu nyumba za umma elfu kumi ziliondoka mikononi mwa umma na hadi leo Watanzania hawajaelezwa zilipatikana shilingi ngapi kwenye mauzo ya nyumba hizo na zilitumika kufanya jambo gani la kuwaondolea wananchi umaskini.
Aidha katika uuzaji wa nyumba za umma Magufuli anatuhumiwa kuwauzia baadhi ya ndugu zake.
Wananchi wanajiuliza kama Magufuli na Lowassa wote walikuwa ni watendaji katika serikali ya CCM, na wote ufisadi umefanyika kwenye maeneo ambayo walikuwa na dhamana, ni kwa nini leo Magufuli anashabikiwa na CCM kuwa ni mwadilifu ili hali Lowassa akipakaziwa ufisadi ?
Aidha, wananchi wanauliza ufisadi kwa Magufuli katika kusimamia kwa niaba ya serikali ya CCM uuzaji kwa bei poa nyumba za umma umetoweka kwa vile tu anagombea Urais kwa tiketi ya CCM na tuhuma za ufisadi kwa Lowassa mkataba wa Richmond umebaki kwa sababu tu ameamua kuondoka CCM na kugombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA –chama kinachowakilisha vyama vinne vya upinzani vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA?
Mfano wa Nne: Ufisadi wa Tegeta escrow 2014, serikali ya CCM ilifisadi bilioni 306. Watuhumiwa wa ufisadi huo walienea ofisi mbali mbali za serikali hadi ofisi kuu ya ya nchi –Ikulu inayopaswa kuwa mahali patakatifu ilihusishwa na ufisadi huo!
Tena wananchi walielezwa jinsi mabilioni ya fedha hizo zilivyokwapuliwa kibabe nyingine zikibebwa kwa magunia na tandarusi mchana kweupe.
Watawala wa CCM waliopaswa kujiuzulu kama Lowassa alivyojiuzulu na kisha kupakaziwa ufisadi tuliona jinsi walivyosafishwa na serikali ya CCM yenyewe!
Wananchi wanajiuliza kama ufisadi wa Richmond haukuwa mkakati wa CCM wa kutumia siasa za maji taka kumtoa Lowassa kafara wa ufisadi kudanganya wananchi kwamba serikali ya CCM siyo fisadi bali fisadi ni Lowassa ni kwa nini Magufuli kwa dhamana yake kama Waziri wa Nyumba alisimamia ufisadi wa nyumba za umma CCM inamuona mwadilifu na Waziri wa nishati Muhongo aliyekuwa na dhamana wakati wa ufisadi wa Tegeta escrow alisafishwa ili hali Lowassa aliyesimamia ufisadi wa mkataba wa Richmond anapakaziwa ufisadi?
Zaidi wananchi wanajiuliza kama chanzo cha ufisadi nchini kama vile Magufuli na CCM wanayotaka kuaminisha umma ni LOwassa na wengine walioondoka CCM, je ni kwa nini serikali ya CCM imekumbwa na ufisadi wa Tegeta escrow miaka saba baada ya Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu?
Hakika ziko fisadi nyingi zilizohusisha viongozi wa serikali ya CCM iwe ni kwenye miradi ya kitaifa au kwenye halmashauri na mikataba ya mali za nchi kama vile madini kuonyesha kwamba umaskini wa wananchi unasababisha na ufisadi wa serikali ya CCM.
Ndiyo sababu kwa kutumia mifano hii minne wananchi wanajiuliza ni kwa nini CCM imtoe Edward Lowassa kafara wa ufisadi ili hali serikali ya CCM ndiyo fisadi?
Kadhalika wananchi wanajiuliza ni kwa nini Edward Lowassa ambaye ameamua kuondoka CCM kutumia haki yake ya kikatiba kutimiza ndoto yake ya kugombea Urais , CCM inamuona tishio na hafai kuwa Rais?
Kama alikuwa hafai kuwa Rais kutokana na ufisadi ilikuwaje alipewa dhamana kubwa ndani ya serikali ya CCM kuanzia uwaziri hadi Waziri Mkuu na akajiuzulu uwaziri mkuu ili kuzuia serikali ya chama chake isianguke kutokana na ufisadi?
Wananchi wanajiuliza hivi tatizo hapa ni ufisadi wa Lowassa kweli au ni CCM kutaka kung’ang’ania madaraka ya kuongoza hata kama wananchi hawakitaki tena chama hicho kiongoze nchi?
Wananchi pia wanajiuliza hivi tatizo ni Lowassa ambaye anao uzoefu mkubwa wa kuongoza serikali na ambaye rekodi yake inaonyesha kuwa ni mchapa kazi au tatizo ni kwa vile anagombea Urais kupitia CHADEM-UKAWA na wananchi wamemkubali ingawa CCM ilidhani umma ungemkataa kutokana na kuchafuliwa kimkakati kwa ufisadi?
Wananchi wanajiuliza kama Magufuli ni mwadilifu kuliko Lowassa na kwamba CCM siyo inayonufaika na ufisadi unaofanywa na watumishi wa serikali yake ni kwa nini CCM wamekataa kuandika Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ili kuweka misingi ya kikatiba kuziba mianya kwa serikali ya chama chochote kuwa fisadi wa fedha na mali za wananchi?
Wananchi wanajiuliza ni kwa nini CCM inahaha kumzuia Lowassa kuwa Rais wa Jamhuri kama CCM haiogopi hatari ya kuachia chama kingine kuingia madarakani wakati nchi haijaweka misingi ya kuzuia serikali kuwa fisadi na hivyo wanaogopa kuwa serikali ya CHADEMA na UKAWA nayo itakuwa fisadi kama ilivyokuwa serikali ya CCM?
Vile vile wananchi wanajiuliza, kama Rais Jakaya Kikwete ambaye mwaka 2005 alipigiwa kampeni na CCM kuwa ni mwadilifu, kama anavyonadiwa Magufuli sasa lakini kwa miaka 10 umaskini wa wananchi umeongezeka –deni la taifa limeongezeka kila Mtanzania anatakiwa kulipa shilingi 800,000/-—je Magufuli atakuwa na ubavu gani wa kuifanya CCM na serikali yake isiendelee kuwa fisadi?
Ni kutokana na hoja hizi ndiyo sababu wananchi wengi wanaona kumchagua Magufuli kuwa Rais wa Tanzania ni kuchagua ufisadi na ni kuchagua mamilioni ya watanzania waendelee na umaskini. HAIKUBALIKI.
Tena wakati mamilioni ya wananchi wanaendelea kuwa maskini watawala wa serikali ya CCM, familia zao, wapambe wao kwenye kampeni na marafiki zao wataendelea kujitajirisha kufuru na kwa kujigawia fedha na mali zinazopaswa kunufaisha Watanzania wote.
Ndiyo sababu wananchi sasa wanahamasishana kutambua kuwa kumchagua Magufuli ni kuichagua CCM na ni kama kumpa tenda ya ulinzi mlizi mwizi!
Wananchi wanaona ni afadhali kuichagua CHADEMA-UKAWA kwa sababu kwanza mgombea wake wa Urais Lowassa huenda akaonyesha uadilifu na uchapakazi wa hali ya juu kuwathibitishia Watanzania kwamba CCM amepakaziwa na kutolewa kafara ufisadi ili CCM iendelee kubaki madarakani bila kujulikana kwamba serikali yake ndiye malkia wa ufisadi nchini.
Wananchi wanatambua kuwa kuirejesha CCM Ikulu kasi ya umaskini itaongezeka kwa wananchi wengi kuaendelea kukosa kipato, kukosa elimu bure na bora hadi chuo kikuu kuondoa adui ujinga na wizi, biashara chafu, uvunjifu wa haki za binadamu na serikali kuwa mbabe, dikteta mminya demokrasia vitaongezeka na hivyo kuvuruga amani ya nchi yetu.
Hivyo ni muhimu serikali ya CCM ikaacha sauti na maamuzi ya wananchi isikike katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba 2015 ili endapo wananchi wataamua kumchagua Lowassa kama Rais wao kupitia CHADEMA inayowakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), waandike Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi na wasipofanya hivyo uchaguzi wa 2010 wananchi wawanyang’anye madaraka.
Katiba mpya siyo tu itampunguza madaraka ya Rais kuhusu uteuzi wa watendaji ikiwa ni pamoja na majaji wa mahakama, bali pia itaweka misingi ambayo mihimili mitatu ya utawala wa nchi —Serikali, Bunge na Mahakama vitakuwa haviingiliani.
Kwa hivyo serikali ya chama chochote ikiiingia madarakani na ikafanya ufisadi itawajibishwa na wananchi nao wataacha na wizi na ujambazi wa kutumia silaha kujitajirisha kama watawala wao wanavyoiba fedha za umma kwa kutumia ujambazi wa kalamu.
Katiba Mpya ya wananchi ikiandikwa, serikali ikifisadi fedha na mali za wananchi itashtakiwa na majaji hawataogopa kuihukumu serikali bila kuipendelea kwa sababu hawatakuwa na woga wa kupoteza ajira.
Hayo ndiyo mabadiliko wanayotaka wananchi wa Tanzania katika kukomesha ufisadi wa kimfumo ili kuepusha ongezeko la wananchi masikini wa kutupa kunakohatarisha amani na umoja wa kweli katika nchi yetu.
Lakini CCM na serikali yake vikitumia rushwa, ubabe na uchakachuaji katika uchaguzi wa tarehe 25 na kushinda uchaguzi, tuendako serikali ya CCM itafanya ufisadi mkubwa zaidi, tena ikitumia ubabe, udikteta na dharau kubwa kwa vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla. Mungu ibariki Tanzania.
Note: Ninaruhusu yeyote anayetaka kutumia , kuchapisha au kusambaza andiko hili afanye hivyo.
------******------------******---------------------*********______
Mwandishi wa makala hii ni Ananilea Nkya ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa TAMWA.
Anapatikana anapatikana kwa E-mail:ananilea_nkya@yahoom.co