MASHEIKH
sita wa Tanzania waliochukuliwa mateka katika Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo (DRC) wameachiwa huru usiku wa kuamkia jana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Liberata Mulamula, alisema Balozi wa
Tanzania nchini DRC kwa sasa yupo njiani kuelekea katika mji mkuu wa
nchi hiyo, Goma kwa ajili ya kuwaona mateka hao.
Alisema taarifa za kutekwa watu hao zilitolewa mwanzoni mwa Agosti
mwaka huu ambapo Serikali ilifanya juhudi ya kufuatilia na kufanya
uchunguzi juu ya taarifa hizo.
Mulamula alisema inasemekena watu hao wa taasisi ya kuhubiri dini ya
Kiislamu walitekwa na kikundi cha waasi ambapo hadi sasa
hakijajulikana.
Alisema watekaji wao walidai wapewe kiasi cha dola za Marekani 40,000
(sawa na Sh milioni 128.7 ) ili wawaachie Watanzania hao huru ambapo
waliwaomba kupunguziwa hadi kufikia dola 20,000.
“Nchi yetu haijawahi kutokea kukamatwa mateka, lakini tunaipongeza
Serikali ya DRC kulifuatilia hili na kutupatia taarifa,” alisema
Mulamula.
Aliwataka wananchi wanaokwenda nchi za ugenini kutoa taarifa katika
ubalozi au Wizara ya Mambo ya Ndani ili waweze kutambua haraka
linapotokea tatizo kama hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya nje Zanzibar, Silima
Kombo Haji, alisema watekaji hao walitumia ujanja wa kupiga simu kwa
ndugu zao pamoja na watu wa karibu na Kijiji cha Goma.
Alisema juzi watekaji hao walikuwa wakipiga simu wakisisitiza kuwa
muda umekwisha, hivyo fedha hizo zipelekwe haraka kabla hawajawadhuru.
No comments:
Post a Comment