19 Sept 2015

Wanachama 100 Wa CCM Watimkia ACT- Wazalendo


Zaidi ya wanachama 100 kutoka CCM, Kata ya Chihanga, Manispaa ya Dodoma wamejiunga na ACT- Wazalendo.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao, Ally Amanzi aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM katika kata hiyo, alisema jana kuwa wamelazimika kuhama kutokana na kufilisika kisiasa.

Amanzi alisema viongozi wa vyama hawaonyeshi kama wanaweza kuleta mabadiliko, badala yake wanafikiria watakavyojilimbikizia mali.

“ACT–Wazalendo tunaimani nayo sisi wakazi wa Kata ya Chihanga, lazima tutapata mabadiliko ya kweli tofauti na vyama vingine vinavyojitokeza kuomba viongozi wao tuwachague,” alisema Amanzi. 
 
Alisema katika chama hicho kuna ubabaishaji mwingi, hali inayochangia wananchi wasipate maendeleo.

Walence Lusingu ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Mkoa wa Dodoma, alisema ACT kimedhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wa kata hiyo.

Lusingu ambaye ni mgombea udiwani katika Kata ya Miyuji, aliwataka wakazi wa kata hiyo kutofanya makosa ya kuchagua viongozi wa vyama vya siasa ambavyo vitawageuza kuwa mitaji pindi vitakapochaguliwa kushika madaraka. 
 
Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, lazima wawe makini katika kusikiliza sera zinazotolewa na wagombea hao, kutokana na wengi wamekuwa wakijinadi kwa kutoa maneno matamu huku wakiwa siyo wakweli.

Mgombea udiwani wa Kata ya Chihanga ambaye alikuwa diwani kupitia CCM kabla ya kuhamia ACT- Wazalendo, Julia Mputu amewaomba wananchi wa kata hiyo, kumpa ridhaa tena ya kumrudisha madarakani ili amalize miradi iliyobaki wakati wa kipindi chake.

Mputu alisema katika kipindi chake cha udiwani, mahitaji ambayo walikuwa wamemtuma mengi ameyafanikisha na machache hajakamilisha.

Aliyataja baadhi ya mambo aliyofanikisha kuwa ni barabara, afya, elimu pamoja na suala ya kilimo.

Hata hivyo, alisema miradi iliyobaki ataikamilisha watakapomchagua katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao.


“Nawaomba mnirudishe nije tumalizie miradi iliyobaki ukizingatia kuwa kazi yangu niliyoifanya kwa kushirikiana na ninyi mmeiona kwa vitendo. Hakukuwa na ubabaishaji wowote,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment