19 Sept 2015

Marekani Yatoa Angalizo uchaguzi Mkuu wa Tanzania


Siku moja tu baada ya Umoja wa Ulaya (EU) kutabiri kuwapo kwa ushindani mkali katika uchaguzi mkuu nchini utakaofanyika Oktoba 25, Serikali ya Marekani imeibuka pia na kutoa angalizo kuhusiana na uchaguzi huo unaohusisha wagombea urais saba wakiwamo Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) linalomilikiwa na Serikali ya Marekani kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea, ilieleza kuwa Bodi ya MCC ina matumaini uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 25 utakuwa huru na wa haki, hasa ikizingatiwa umuhimu mkubwa ambao MCC inauweka katika haki za kidemokrasia. 
 
Kadhalika, taarifa hiyo imemkariri Balozi wa Marekani nchini, Childress akisema (Marekani) wanatambua rekodi ya Tanzania katika kukuza demokrasia na kwamba, wanaunga mkono na kusaidia jitihada endelevu za Tanzania katika kuimarisha taasisi zake za kidemokrasia.

“Tunatarajia kuona uchaguzi ulio huru, wa haki, wa amani na ambao utawasilisha matakwa ya watu wa Tanzania,” alisema Balozi Mark Childress. 
 
Taarifa hiyo ya Marekani kuhusiana na uchaguzi mkuu nchini inatokana na mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi ya MCC iliyokutana juzi kujadili masuala mbalimbali yakiwamo ya utoaji wa misaada kwa Tanzania. 


Mbali na Dk. Magufuli na Lowassa anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF), wagombea wengine wa nafasi ya urais wanaoendelea na kampeni kwa nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete ni Fahmy Dovutwa wa UPDP, Hashim Rungwe wa Chaumma, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Chifu Lutasola Yemba wa ADC

No comments:

Post a Comment