Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, akizungumza jijini Dar es Salaam jana.
WADHAMINI
wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kampuni ya mawasiliano ya
Vodacom Tanzania, wamezitakia kila la heri timu zote 16 zinazoshiriki
ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Jumamosi hii kwenye viwanja mbalimbali
nchini.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian
Ferrao, alisema kuwa ni fahari kubwa kwao kuona msimu mpya wa ligi hiyo
unaanza hivyo kutoa fursa kwa wapenzi wa soka nchini na kwingineko
kupata burudani.
Alizitaka
timu zote pamoja na mchezaji mmoja mmoja, kucheza kwa kufuata sheria
zote 17 za soka ili kuutendea haki mchezo huo, lakini pia mashabiki
ambao wamekuwa wakimiminika kwa wingi viwanjani kuzishabikia timu zao.
Ferrao
aliwaonya viongozi, wachezaji na hata waamuzi kujiepusha na vitendo
vyovyote vinavyoweza kuathiri matokeo ya mchezo husika, zaidi ikiwa ni
rushwa na ushirikina ambao mara nyingi umekuwa ukihusishwa katika
kupunguza uhondo wa soka kwa wachezaji kutojituma uwanjani wakiamini
‘ushindi ni lazima’.
“Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inapoanza mwishoni mwa wiki hii,
wachezaji wa timu zote shiriki, ni vema wakatambua kuwa Vodacom
inawajali ndio maana tumeongeza udhamini kutoka Sh bilioni 1.8 hadi
bilioni 2.3 ili kuifanya ligi kuwa na msisimko wa aina yake, lakini pia
kuboresha maisha ya wachezaji,” alisema.
Juu ya
udhamini wao wa miaka mitatu katika ligi hiyo, Ferrao alisema kuwa
wameongeza dau kwa kuwa timu zimeongezeka kutoka 14 msimu uliopita hadi
16 msimu huu, lakini pia wakifanya hivyo ili kuiboresha na kuongeza
ushindani miongoni mwa wachezaji na timu kwa ujumla.
Ferrao
aliwataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi viwanjani
kuzishangilia timu zao ili kuwapandisha mzuka wachezaji waweze kujituma
kadri ya uwezo wao na kupata ushindi.
Timu
zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa watetezi Yanga, Azam na Simba za Dar
es Salaam, Mbeya City na Prisons (Mbeya), Toto Africans (Mwanza),
Kagera Sugar (Kagera), Mwadui na Stand United (Shinyanga), Coastal
Union, African Sports na Mgambo Shooting (Tanga), Mtibwa Sugar
(Morogoro), JKT Ruvu (Pwani), Ndanda FC (Mtwara) na Majimaji (Ruvuma).
Kwa
mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, kesho Simba itavaana na African Sports
kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Azam watawakaribisha Prisons (Azam
Complex), JKT Ruvu na Majimaji (Majimaji, Songea) na Mgambo watakuwa
wageni wa Ndanda (Nangwanda Sijaona).
Mbeya
City watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar (Sokoine), Mwadui wataifuata Toto
African (Kirumba), Stand Utd wataikaribisha Mtibwa (Kambarage), wakati
mechi nyingine itachezwa Jumapili kwa Yanga kuikaribisha Coastal Union
(Uwanja wa Taifa)
No comments:
Post a Comment