Vita ya makocha sita wa Ulaya Ligi Kuu - LEKULE

Breaking

12 Sept 2015

Vita ya makocha sita wa Ulaya Ligi Kuu


kocha wa Yanga Hans van Der Pluijm
LIGI Kuu Bara inaanza leo huku gumzo likiwa ni uwezo wa makocha sita kutoka Ulaya ambao wanaandika historia ya kuzifundisha timu za ligi hiyo kwa pamoja ndani ya msimu mmoja.
kochaDylanKerrKocha wa Simba Dylan Kerr
Timu sita za ligi kuu zinafundishwa na makocha raia wa nchi za Ulaya ambao ni Hans van Der Pluijm wa Yanga raia wa Uholanzi, Dylan Kerr (Uingereza, Simba), Stewart Hall (Uingereza, Azam FC) na Patrick Liewig raia wa Ufaransa.
Stewart Hall
Kocha wa Azam, Stewart Hall
Wengine ni Martin Grelics wa Toto Africans raia wa Ujerumani na Mika Lonnstorm wa Majimaji raia wa Finland. Wote wameshaanza kazi na katika vikosi vyao na leo Jumamosi watakuwa katika mitihani isipokuwa Pluijm. Kerr ataiongoza Simba dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga, na tayari amejitamba kushinda mchezo huo wa kwanza kwake katika ligi kuu. “Tupo vizuri na kitu pekee tunachosubiri ni kuingia uwanjani kutekeleza kile tulichojifunza kwa muda wote,” alisema Kerr ambaye anasifika kwa soka la kasi na la pasi fupifupi.
Hall yeye ataiongoza Azam katika mchezo dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam ambapo ametamba kufanya vizuri huku akitumia rekodi ya kuchukua ubingwa wa Kombe la Kagame bila kufungwa hivi karibuni. “Tunahitaji kujituma ili kuweza kushinda mchezo huu, naamini mchezo utakuwa mgumu na wa kiushindani, lakini kwa upande wa wachezaji wangu safu zote zipo imara,” alisema Hall.
Grelics wa Toto na Lonnstorm wa Majimaji wenyewe hawakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema wanasubiri kucheza mechi za kwanza ili kujua ligi ilivyo na baada ya hapo wanaweza kuwa na mwanga na ligi ya Tanzania. Toto itacheza na Mwadui FC nyumbani CCM Kirumba wakati Majimaji itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Majimaji kucheza na JKT Ruvu.
Kocha wa zamani wa Simba, Liewig atakuwa nyumbani CCM Kambarage akiiongoza Stand United dhidi ya Mtibwa Sugar. Mzungu mwingine ambaye ni bingwa mtetezi, Pluijm kesho Jumapili ataiongoza Yanga dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. “Mechi ya kwanza siku zote inakuwa na ‘tension’ kubwa, hasa kwa wachezaji na mashabiki, lakini kama unavyojua siku zote sisi, tunahitaji kupata pointi zote na kusonga mbele zaidi,” alisema Pluijm.
Katika mechi nyingine za leo, Ndanda FC itakuwa nyumbani kucheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. Mbeya City itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

No comments: