Tume ya Uchaguzi yalaani mauaji wakati wa kampeni Tarime.....Yaliomba Jeshi la Polisi Kuchunguza Taarifa za Vijana 1500 Waliopewa Mafunzo ya Kijeshi - LEKULE

Breaking

18 Sept 2015

Tume ya Uchaguzi yalaani mauaji wakati wa kampeni Tarime.....Yaliomba Jeshi la Polisi Kuchunguza Taarifa za Vijana 1500 Waliopewa Mafunzo ya Kijeshi



Kwa masikitiko na mshangao mkubwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea taarifa ya kutokea kwa mauaji katika Kijiji cha Mangucha Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati wa Kampeni za Uchaguzi ambapo Bwana Mwita Bhoke Waitegi aliuawa.

Tume inakemea vikali na kwa nguvu zote ukiukwaji wa Maadili unaopelekea uvunjifu wa amani na kusababisha vurugu ambazo hatimaye wakati wa Kampeni mauaji yametokea.

Kwa mujibu wa Taarifa zilizopokelewa na Tume, pamoja na mambo mengine, kwa kiwango kikubwa kifo kilisababishwa na fujo, vurugu na kurupushani kati ya wafuasi wa Vyama vya CCM na CHADEMA.
 
 Vurugu na fujo hizo ni kinyume kabisa cha Maadili ya Uchaguzi ya 2015 yaliyotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa vilivyosajili tarehe 27/08/2015.

Kwa mujibu wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 kifungu cha 2.2 (a) Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea wao hawatakiwi kufanya fujo au kusababisha vurugu ya aina yoyote katika mkutano wa Chama kingine, (b) Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea wao hawatakiwi kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjaji wa amani, au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu au maumbile, kwenye mikutano ya Kampeni.

Aidha, Maadili hayo kifungu (c) kinaeleza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kuwa na/au kubeba silaha yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za jadi au zana yoyote inayoweza kumdhuru mtu katika mkutano wa Kampeni au mkusanyiko wowote wa kisiasa, na kifungu (d) kinaeleza kuwa hairuhusiwi kuwa na/au kubeba sanamu, kinyago au kitu chochote ambacho kinaonyesha kudhalilisha, kukebehi au kufedhehesha Chama kingine cha Siasa au Kiongozi wake au Serikali katika mkutano au mkusanyiko wowote wa Kisiasa.

Kwa vile kutokana na kutozingatiwa kwa Maadili ya Uchaguzi, 2015 kifo kimetokea na baadhi ya wananchi, wanachama wa Vyama hivi vya Siasa kuumia, Tume kwa mara nyingine inakumbusha na kusisitiza Vyama vyote vya Siasa na Wanachama wao kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya 2015.

Tume pia imepata taarifa ya kuwepo kwa baadhi ya Vyama vya Siasa ambavyo vinaandaa vijana zaidi ya 1500 na kuwapa mafunzo ya kijeshi ili kufanya vurugu wakati wa Uchaguzi. 
 
Taarifa hizo japo ni za upande mmoja Tume inaliomba Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo na kuchukua hatua ili kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani. Hili nalo, Tume inalikemea kwa nguvu.

Chama chochote hakiruhusiwi kuwa na vikundi vya aina hii. Ni kinyume cha Sheria na Maadili ya Uchaguzi.

Imetolewa na:

Mh. Jaji (Mst.) Damian Z. Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Tarehe 18 Septemba, 2015

No comments: