Sakata
la madeni ya walimu limezidi kuchukua sura mpya baada ya serikali
kusema haidaiwi na kwamba imebaini kuwapo kwa majina hewa ya walimu
zaidi 4,000 yaliyowasilishwa kwa ajili ya malipo.
Imesema
imegundua hivyo baada ya kufanya uhakiki wa deni la Sh. bilioni 19.6
lililowasilishwa na walimu baada ya kuwalipa madai yao kwa mara ya
mwisho mwaka 2013.
Kwa
mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile,
baada ya kuhakiki madeni hayo mwaka jana, serikali imegundua deni halisi
inalodaiwa na walimu ni Sh bilioni 5.6 tu.
Alisema endapo serikali isingefanya uhakiki wa deni hilo na kulilipa ingeingia hasara ya Sh. bilioni 14.
Alisema
katika uhakiki huo, wizara hiyo imebaini kulikuwa na deni hewa kubwa la
mwalimu mmoja wa Halmashauri ya Tunduru Mkoani Lindi Sh. milioni 500 na
kwamba baada ya kuhakiki imegundua deni lake halali ni Sh. 500,000 tu.
Dk. Likwelile alisema kwa madeni ya mwaka jana, serikali imelipa walimu Sh. bilioni 5.6 baada ya kufanya uhakiki.
“Katika uhakiki tumebaini kuwapo udanganyifu wa fedha kwa walimu kujiongezea huku wengine wakidai deni la aina moja mara nne,” alisema.
Dk.
Likwelile alitaja sababu za serikali kukataa kulipa baadhi ya madai ya
walimu yaliyowasilishwa ni pamoja na kukosa vibali au vielelezo, madai
mengine kuwa yameshalipwa, mishahara iliyowasilishwa kama madai yasiyo
ya mishahara, baadhi ya walimu kutotambuliwa na halmashauri, baadhi ya
walimu kutokuwa na madai katika majalada na makosa ya ukokotoaji na
uandishi.
No comments:
Post a Comment